SABABU YA KUFUNGWA JELA KWA MKURUGENZI WA TBS EKELEGE HIZI HAPA LIVE!!
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela
Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles
Ekelege na kumwamuru kurejesha Dola za Marekani 42,543 (Sh68,068,800).
Hakimu
Mmbando alisema katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulithibitisha
mashtaka yote yanayomkabili Ekelege pasipo kuacha shaka na kumhukumu
kifungo hicho.
Mmbando
alisema viongozi wapo kwa ajili ya kulinda masilahi na rasilimali za
nchi ili wananchi waweze kuifurahia keki ya Taifa na siyo kufuata
matakwa yao.
Alisema
kiongozi kama Ekelege aliaminiwa na kuteuliwa na Rais ili aweze
kuiongoza TBS ambayo ni sehemu ya chanzo cha mapato ya nchi, hivyo
kuzembea kwake na kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha, hapaswi
kuonewa huruma ili iwe fundisho kwa viongozi wengine.
Katika
shtaka la kwanza la kutumia madaraka yake vibaya kwa kuziondolea
asilimia 50 ya ada ya utawala, Kampuni za Jaffar Mohamed Ali na Quality
Motors, Ekelege alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.
Katika
shtaka la pili la kuondoa ada za kampuni hizo bila idhini ya Baraza la
Utendaji kinyume na utaratibu wa TBS pia alihukumiwa kifungo cha mwaka
mmoja jela na katika shtaka la tatu la kusababisha hasara ya kiasi hicho
cha fedha alifungwa tena kifungo kingine cha mwaka mmoja jela.
Hakimu
Mmbando alisema vifungo hivyo vitakwenda pamoja, hivyo mshtakiwa huyo
atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na kurejesha Sh68,068,800
anazodaiwa kulisababishia shirika hilo hasara kwa uzembe.
Kabla
ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machulya alisema kwa kuzingatia
uzito wa mashtaka aliyotenda Ekelege na alivyoshindwa kuitumikia dhamana
aliyopewa, anastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa viongozi
wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Machulya aliiomba mahakama wakati ikifikiria kutoa adhabu kwa Ekelege izingatie sheria ya uhujumu uchumi.
Wakili
aliyekuwa akimtetea Ekelege, Majura Magafu aliiomba Mahakama impunguzie
adhabu mteja wake kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, ana familia ya mke,
watoto na wazee wanaomtegemea.
Utetezi wa Ekelege
Katika
utetezi wake, Ekelege alikana kusababisha hasara kwa kutoa msamaha,
akisema hali hiyo ilitokana na udanganyifu uliofanywa na kampuni husika.
Alidai
kuwa kampuni hizo zilidanganya na kusababisha kutoa uamuzi mwingine
ambao haukuwa sahihi na bodi ya wakurugenzi ya TBS ilipoitishwa
iliridhia kuwa msamaha huo haukutolewa kwa makusudi.
Alisema
kwa kuwa TBS haikuwa na historia ya kutoa msamaha hiyo na kwa kuwa
ilikuwa mara ya kwanza na kampuni hizo hazikuwa na uaminifu, aliiomba
Mahakama imwachie huru.
Akijitetea,
alisema kampuni ya Jaffar Mohamed Ali ilipata msamaha baada ya
kuwasilisha maombi yake ikidai kuwapo kwa ushindani uliotokana na wakala
mwenzake, Total Otomotive Services, aliyekuwa akifanya mchezo mchafu wa
kuvuta wateja kwa kutokagua viwango vya ubora wa magari yao na kuwapa
vyeti vya ubora.