MAITI AZIKWA KIMAAJABU!
Na Waandishi Wetu
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida na
kushangaza, wananchi wa Mbezi Msakuzi Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam, walisusa na kuondoka makaburini kwa kile kilichodaiwa kuwa maiti
ya Michael Krisantu (pichani) waliyotarajia kuizika iliwekwa ndani ya
jeneza kimaajabu.
Tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika
Makaburi ya Makamba Msakuzi, Mbezi jijini Dar es Salaam ambapo wananchi
hao waligundua kuwa maiti ya kijana huyo iliweka ndani ya jeneza
kinyume na utaratibu uliozoeleka yaani kichwa chake kilielekezwa sehemu
ya miguu na miguu ilielekezwa sehemu ya kichwa.
Kama hiyo haitoshi, maiti hiyo badala ya
kuviringishwa sanda nyeupe, ilitumika sanda nyeusi kitu kilicholeta
tafsiri tofauti miongoni mwa waombolezaji.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa,
kabla jeneza lenye mwili kutumbukizwa kwenye kaburi kulitokea mvutano
mkubwa baina ya wanandugu na waombolezaji.
Imeelezwa kuwa, waombolezaji hao waliwataka
wanandugu wafuate taratibu zilizozoeleka katika jamii wakati wa
kuzika.Hata hivyo, ndugu wa marehemu hawakuwasikiliza na kudai kwamba
walikuwa wanafuata mila na tamaduni za kabila lao (jina la kabila
linahifadhiwa kwa sababu maalum).
Wanandugu hao wakaamua kushusha jeneza
lenye mwili kaburini na walipoanza kuzika waombelezaji walikuja juu na
kulitoa jeneza kaburini hali iliyosababisha kutokea kwa vurugu kubwa.
“Vurugu hizo zilisababisha wanawake
waliokuwa makaburini kutimua mbio na wanaume wakasusa na kuwaacha
wanandugu waendelee kumzika ndugu yao,” alisema shuhuda wa tukio hilo
kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.
Marehemu Michael Krisantu enzi za uhai wake.
Habari zinasema kuwa, kutokana na utata huo, hata mchungaji
aliyepaswa kuendesha ibada ya mazishi aliondoka bila kutoa huduma ya
kiroho.
Mmoja wa wanandugu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la
Victor, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo hakuweza kusema chochote
badala yake alikuwa akibubujikwa na machozi.