KENYA YATEKETEZA KILO 370 YA HEROINE
Serikali ya Kenya imeharibu
shehena ya mihadarati aina ya Heroine iliyokuwa imenaswa katika bahari
hindi huko Mombasa mwezi mmoja uliopita.
Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza
hapo jana kuwa shehena hiyo itaharibiwa na kuzamishwa baharini na meli
iliyokuwa imeibeba
Uharibifu huo wa kilo 370 za heroine
ya gharama za ya zidi ya dola milioni 16 za Marekani ulifanyika mwendo
wa saa kumi saa za Afrika Mashariki umbali wa maili kumi na nne baharini
kutoka katika bandari ya Mombasa.
Maafisa wa jeshi la wanamaji walilipua shehena hiyo na kukasikika
mlipuko mkubwa baharini kisha meli hiyo ya kigeni aina ya MV Al Noor
ikazamishwa.
Walioshuhudia uharibifu huo walijumuisha maafisa
wakuu wa polisi nchini Kenya, wale wa kitengo cha kukabiliana na
mihadarati, wakuu wa idara za ujasusi wa mataifa kumi na tatu waliokuwa
Mombasa kuhudhuria mkutano wa usalama na jeshi la wanamaji.
Awali mahakama kuu ya Mombasa ilikataa kutoa agizo la kuharibu meli iliyokuwa imebeba shehena hiyo.
Jaji aliyeisikia kesi hiyo iliyokuwa
imewasilishwa na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma alisema kuwa
hakutaka kuonekana kukinzana na mahakama ya chini ambayo ilikuwa
imeelekeza tu shehena hiyo ya heroine iharibiwe.
Akitoa onyo kali kuhusu matumizi ya dawa za
Kulevya rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa hatakubali Kenya kuwa sehemu ya
kusafirisha dawa za kulevya kutoka mataifa mengine.
Si mara ya kwanza shehena ya dawa za kulevya
kunaswa Mombasa na hatua hii inaonekana ni moja ya jitihada za kupambana
na matumizi ya dawa hizo.
Mji wa Mombasa na maeneo jirani ni baadhi ya
sehemu ambazo zimeathiriwa pakubwa na matumizi ya dawa za kulevya
hususan kwa vijana ambao wamekabiliwa na uraibu wa dawa hizo na kupata
madhara ya kiafya.