Dk. John Magufuli Nae Atangaza Nia yake ya Kuwania Tonge la Urais wa Tanzania 2015, Adai Anazo Sifa Zote

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kwa wanachama wake wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini, ameona hana budi kutangaza rasmi azma yake.

Dk. Magufuli, mmoja wa mawaziri ambao kwa muda mrefu wamehusishwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo, alisema anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga na kupigiwa kura.

Alitangaza azma yake nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu bungeni, jana asubuhi.
Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo, mara moja alisema: “Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.

“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza.

Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea urais’. Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema siku ya kuchukua fomu ataitangaza baadaye pindi akishakamilisha taratibu za namna ya kuanika hadharani mambo anayokusudia kuyatekeleza endapo wana CCM watampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini