Matapeli wavamia usajili wa wachezaji




Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope 



Na Oliver Albert

Dar es Salaam. Wakati usajili wa wachezaji nchini ukiendelea kushika kazi, kumezuka wimbi la watu wanaojifanya mawakala, wawakilishi wa wachezaji, kumbe ni matapeli, gazeti hili limebaini.



Awali, mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe aliliambia gazeti hili kuwa matapeli hao wanaojifanya mawakala wamekuwa wakishiriki kupanga bei na hata mikataba ya wachezaji.


Mawakala hao uchwara, Hanspoppe (pichani)amedai hawana leseni zinazotambuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au lile la Kimataifa (Fifa), wamekuwa wakiwapotosha baadhi ya wachezaji na kuwaingiza katika mizozo na klabu.



Alisema viongozi wa soka nchini hawana budi kuwa makini na mawakala wa wachezaji walioanza kujitokeza kipindi hiki cha usajili, wakipanga bei za wachezaji bila kufuata utaratibu.


Aliongeza kuwa kipindi hiki ambacho wachezaji wengi wanaongeza mikataba na baadhi kusajiliwa, kumejitokeza kundi hilo la watu wanaojiita mawakala, hupanga bei za wachezaji wakiwa hawatambuliki na mamlaka zinazosimamia michezo na klabu anayochezea mchezaji.


Kauli hiyo ya Hanspoppe imetolewa wakati klabu yake ikiwa na mzozo na kiungo wake, Ramadhani Singano ‘Messi’, ikimtaka apeleke klabuni hapo nakala halisi ya mkataba wake ili kumaliza kelele na kumaliza ubishi uliopo baina ya pande hizo mbili.


Singano, ameingia katika vita na uongozi wa timu hiyo kwa madai kuwa wameghushi mkataba wake, akidai mkataba huo unamalizika mwaka huu, wakati klabu iking’ang’ania kuwa unamalizika 2016.


Mchezaji huyo chipukizi amelalamika kwenye vyombo vya habari kuwa, Simba imecheza mchezo mchafu kumwongezea mkataba kwa mwaka mmoja ambao hautambui na mkataba wake halali uko TFF.


Hata hivyo, Hanspoppe alimtaka Singano kupeleka mkataba huo anaodai ni halali kwenye uongozi wa klabu hiyo ili kulinganisha na mkataba uliopo klabuni na ule wa TFF ili ukweli ujulikane.



Pia, Hanspoppe alisisitiza kuwa mkataba wa Singano unamalizika mwakani na si mwaka huu kama ambavyo amekuwa akisema mchezaji huyo.


“Alete mkataba alionao maana, kawaida kuna kuwa na nakala tatu; yetu, yake na ya TFF. Sasa alete yake, sisi tutoe yetu na itaangaliwa na TFF ili kuangalia wapi kuna tatizo.


“Tena, alete mkataba halisi na siyo nakala kwani unapokuwa na nakala mtu yeyote anaweza kuichezea. Hivyo, hatutakubali kwani ili jambo kulimaliza ni rahisi kuliko kuendelea kukuzwa kwa sababu mikataba yote ipo,” alisema Hanspoppe.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini