IMAMU: NIMEMWAGIWA TINDIKALI KUTETEA MALI ZA MSIKITI

Na Musa Mateja
UNYAMA wa kutisha! Bwana mmoja ambaye ni imamu, aliyefahamika kwa jina la Mustafa Omar Mustafa, mkazi wa Ghana, Kata ya Nyamanoro jijini Mwanza, amefanyiwa unyama wa hali ya juu kwa kumwagiwa tindikili na watu wanaosadikiwa kuwa ni waumini wenzake, kisa kulinda mali za msikiti wao uliopo katika mtaa huo wa Ghana. Uwazi linakupa habari kamili.


Mustafa Omar Mustafa, anayedaiwa kumwagiwa tindikali.
ILIKUAJE?
Akizungumza na mwandishi wetu kwa masikitiko Mustafa alisema kuwa, tukio hilo la kinyama alifanyiwa majira ya saa mbili kasorobo usiku, Jumapili ya Agosti 31, mwaka jana akiwa nyumbani kwake Ghana.
“Nilikuwa katika hali ya furaha na familia yangu, sikuhisi kabisa hatari ambayo ilikuwa inakuja kutokea katika maisha yangu. Tukiwa hatuna hili wala lile, tulishitukia kundi la watu likivamia nyumba yangu ndipo waliponitendea unyama huu na kutoweka,” alisema.
AKIMBIZWA HOSPITALI YA MKOA SEKOU-TOURE
 “Baada ya unyama huo familia yangu na jamaa wa karibu kwa haraka walinikimbiza katika kituo kidogo cha polisi cha kata hiyo ambapo nilipata kibali cha matibabu (PF3) na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-toure, ambapo nilipokelewa na kuingizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.“Katika chumba hicho nilikaa kwa muda wa siku sita nikahamishiwa katika chumba cha wodi za kawaida.”
Mustafa akionyesha jeraha alilolipata mkononi.
MATIBABU YASHINDIKANA AHAMISHIWA CCBRT
“Baada ya hali yangu kuzidi kuwa mbaya, madaktari wa hospitali hiyo walinishauri kufanya utaratibu wa kwenda kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya CCBRT Dar ambayo inasifika kwa kutoa huduma nzuri ya matibabu ya macho.
“Kama unavyoona sehemu kubwa niliyoathirika na tindikali ni usoni, kifuani na mgongoni! Mwanzoni kabisa macho yote hayakuwa yanaona ndipo nilipohamia CCBRT, ambapo angalau nimeweza kupata matibabu, namshukuru Mungu sasa jicho moja la kulia linaweza kuona kwa mbali.
KISA CHA KUMWAGIWA TINDIKALI
 “Kabla ya tukio hilo katika msikiti wetu kulikuwa na mgogoro kati ya waumini na viongozi wa msikiti.
Hatukuwa tunawataka ambapo baada ya mvutano wa muda mrefu uliosababisha kufikishwa  mahakamani baadhi ya watu, uchaguzi wa viongozi wengine ulifanyika chini ya uangalizi maalumu wa mahakama, baada ya kupatikana viongozi wapya nilipendekezwa kuwa imamu na nikawa naongoza sala za asubuhi.
Jeraha la kifuani.
“Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele, nilianza kujihusisha na shughuli mbalimbali za msikiti ikiwemo kufanya usafi wa mazingira  na kutunza baadhi ya rasilimali jambo ambalo lilionekana kutolifurahisha kundi la baadhi ya watu ambao hawakuwa wanaupenda huo uongozi mpya, ambapo kwa kile walichokiita kunikomesha ndipo walipoamua kunimwagia tindikali.
MSAADA
“Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi niliyonayo, nawaomba Watanzania watakaoguswa na matatizo yangu kunisaidia ili niweze kupata huduma ya matibabu zaidi kwani hali yangu kiuchumi kwa sasa ni mbaya sana.
“Nawashukuru sana wote ambao wamenisaidia mpaka angalau nimekuwa katika hali hii, japo hali yangu bado haijawa vizuri sana hasa kimaisha, maana nimeshatumia fedha zangu zote kwa ajili ya matibabu na leo hii nafikia hatua ya kuomba kwa kuwa familia inanitegemea na haina namna tena, mtaji wangu wote umeishia katika matibabu.
“Kabla ya kufanyiwa unyama huu nilikuwa wakala wa mitandao ya simu na sasa changamoto yangu kubwa ni hali ya hewa ya jijini Dar es Salaam kuwa ya joto sana, hivyo napata maumivu sana kwenye majeraha yangu.
Jeraha la mgongoni.
MACHO
 “Hivi sasa matibabu ya macho bado yanaendelea ingawa nimeambiwa nirudi tena mwezi ujao (Juni) ambapo nimepewa uhamisho kwenda katika Hospitali ya Ocean Road kwa ajili ya kushughulikia tatizo la ngozi ambayo nayo imeharibika vibaya.
“Nilikwenda katika hospitali hiyo nikaambiwa kumuona daktari tu, natakiwa kutoa shilingi elfu hamsini, kiasi ambacho kwa sasa ni kikubwa sana kwangu maana nakosa hata shilingi mia mfukoni.“Ninayoyasema hapa ni rahisi kwa asiye jua hali yangu kuona kama natania ila ukweli ni kwamba hata fedha ya kwenda hospitali kumuona huyo daktari sina.
“Nawaomba Watanzania wanisaidie ili niweze kumuona daktari kisha nipate nauli ya kurudi Mwanza kukaa na familia yangu japokuwa siwezi kuihudumia. Changamoto ni kwamba baada ya mwezi natakiwa kurudi Dar kwa matibabu ya macho na ngozi.
“Nampongeza sana Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Eric Shigongo kwa kuwa nami bega kwa bega tangu nipate tatizo hili na hakika yeye ni mtu mwenye upendo wa dhati, pia nawashukuru wote ambao wanaendelea kunijulia hali,” alisema Mustafa huku akilengwalengwa na machozi.
 Aliyeguswa na habari hii awasiliane naye kwa namba 0752 362 221, kutoa ni moyo.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini