Lowassa aitikisa Arusha......Watu wafurika, Wakosa vyumba Walala katika Magari, wengine wajiapiza Kulala Uwanjani....... Mkuu wa Majeshi mstaafu naye Atinga, fulana zenye Picha yake Zapanda Bei


NYUMBA za kulala wageni katika Jiji la Arusha na viunga vyake zimeanza kufurika kutokana na makundi ya watu yanayowasili jijini hapa kushuhudia mwanzo wa ‘Safari ya Matumaini’ ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa  Monduli Edward Lowasa, anayoianza rasmi leo.
Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa makada wa CCM walioonyesha nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho anatarajiwa kutangaza nia leo kuanzia saa 8 mchana katika Uwanja wa Sheikh Amri Abed Kaluta Jijini hapa. 
Mpekuzi imeshuhudia pilikapilika katikati ya Jiji, Mitaa ya Kaloleni, Makao mapya, Levolosi na maeneo ya pembezoni ambako kuna nyumba za kulala wageni, baadhi ya watu wakiulizia vyumba ambapo katika nyumba nyingi kuna kibao kinachosomeka ‘vyumba vimejaa’.
Baadhi ya wageni hao ambao walizungumza na Mpekuzi kwa sharti la kutotaja majina yao walisema pamoja na kukosa vyumba wako tayari kulala nje hadi watakapoianza ‘safari ya matumaini’ pamoja na Lowassa.


“Kukosa vyumba si tatizo kwetu, tutalala hata uwanjani,tumesubiri sana siku hii ambayo Mzee (Lowassa) alianza kuitaja tangu Mwaka 2013, tunamshukuru Mungu imefika na tutaanza safari ya matumaini pamoja naye,” alisema mmoja wa wageni hao.
Kujaa huko kwa nyumba za kulala wageni, hoteli baadhi ya watu usiku wa kuamkia jana na leo walilazimika kulala kwenye magari.
Taarifa kutoka kambi ya Lowassa zinaeleza kuwa, watu wengi kutoka kada mbalimbali, wanatarajia kushiriki mkutano huo ambao Waziri Mkuu huyo wa zamani pamoja na mambo mengine atautumia kueleza matarajio yake endapo chama chake kitamteua kugombea urais.
Kwa mujibu wa taarifa hizo miongoni mwa waliokwisha wasili jijini humo ni pamoja na Wajumbe wa NEC wa chama hicho wapatao 187 huku wengine 93 wakitarajia kuwasili usiku wa kuamkia leo.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na wajumbe hao pia wenyeviti wa mikoa 23 nchini nao watakuwepo leo katika uwanja huo wa Amri Abeid Kaluta.

Zaidi wazee maarufu akiwemo Kingunge Ngombale Mwiru, Pancras Ndejembi, Kanali Mwisongo, na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Mirisho Sarakikya nao pia wanatajwa kushiriki tukio la leo.
Mbali na kufurika kwa wageni katika Jiji la Arusha wanaosubiri kwa hamu hotuba itakayotolewa na Lowassa hii leo, pia mavazi ikiwamo sare za CCM  zenye utambulisho maalumu kwa ajili ya siku hiyo nazo zimepanda bei mara dufu.
Wajasiriamali wanaouza fulana zenye picha na maandishi yanayomtaja Lowassa ambazo zilikuwa zikiuzwa kati ya sh.10,000 na 15,000 sasa zinauzwa kwa kati ya Sh.20,000 na 25,000 hata hivyo pamoja na kupandishwa bei bado zimekuwa adimu.
 “Fulana hii shingo ya mduara ni Sh. 20,000 na hii ya shingo ya v (form six) nauza Sh.25,000 kaka karibu na zimebaki chache sana mpaka tuagize zingine shughuli itakuwa imeshafanyika bora uchukue hii,”alisema mmoja wa wajasiriamali aliyekuwa ametandaza nguo hizo na sare za Chama katika moja ya mitaa jijini hapa.

Mbali na kukamilika kwa maandalizi yote ya hotuba muhimu inayosubiriwa kwa hamu na Watanzania ya ‘Safari ya matumaini’ kumekuwa na shamra shamra kila kona ambapo kila mtaa watu wamekaa vikundi wakijadili kwa heri na wengine kwa shari ‘Safari hiyo ya Matumini’.

Hali  ya  Uwanja
 Maandalizi  katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa yalianza  tangu juzi mapema asubuhi.

Tofauti na miaka yote pengine tangu uwanja huo ujengwe unaweza kuwa haujawahi kupambwa kama ambavyo ulianza kupambwa jana ambapo kazi hiyo ilitarajiwa kukamilika saa 8. mchana jana.
Baadhi ya mapambo yaliyokuwa na rangi za Chama cha Mapinduzi (CCM), yalionekana kutawala zaidi katika viwanja hivyo huku mahema kwa ajili ya tahadhari ya mvua na jua yakiwa yamefungwa.
Mbali na mahema hayo pia magari makubwa ya mizigo yalikuwa yakipishana kuingiza vifaa mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo ya upambaji lakini pia tayari kwa shughuli nzima ya kesho.
Vyombo  vya  Habari
Mkutano huo wa kutangaza nia wa Lowassa kama ambavyo umekuwa ukitangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari unatarajiwa kurushwa moja kwa moja pia na vyombo vya habari kutoka ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya vyombo vya habari kutoka ndani ambavyo vitarusha moja kwa moja mkutano huo ni pamoja na  Televisheni ya ITV,Channel Ten, Clouds TV, EATV, ambapo kwa upande wa redio ni Clouds FM, Magic FM,na East Africa Redio.
Lakini pia vyombo vya habari kutoka nchini Kenya navyo vipo Mkoani Arusha tayari kwa kufuatilia mkutano huo.
Vyombo hivyo ni pamoja na Televicheni ya Citizen, Nation na gazeti la The Standard.
Kuanza kwa Safari hiyo ya Matumaini ya Lowassa, kumekuja baada ya kukamilika kwa adhabu aliyopewa sambamba na makada wenzake ndani ya chama baada ya kudaiwa kuanza kampeni na ushashawishi kabla ya wakati.
Makada waliokuwa wamepewa adhabu na CCM mbali na Lowassa alikuwemo pia, Benard Membe, Steven Wassira, William Ngeleja, January Makamba na Frederick Sumaye.

Tayari vikao vya juu vya CCM vimekwisha toa ratiba kamili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, Mwaka huu ambapo kwa upande wa urais zoezi la uchukuaji fomu kwa ngazi ya urais litaanza Juni 2 mwaka huu.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini