ZITTO KABWE Atema Cheche Tanga...Ajigamba Kuwang'oa MAWAZIRI 13 Wa CCM

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kama angekuwa ni msaliti na kibaraka wa Chama cha Mapinduzi (CCM), asingeweza kuongoza mapambano ya kuwang’oa mawaziri 13 kwa miaka mitatu katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete. 

Aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mabawa uliolenga kukitangaza rasmi chama chake kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na vitongoji vyake. 

Zitto alisema mwaka 2012 aliongoza mapambano ya kuwang’oa mawaziri wanane wakati mwaka 2013 walijiuzulu mawaziri wanne kwa kashfa ya Oparesheni Tokomeza, wakati mwaka jana, mawaziri watatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walilazimika kuachia ngazi kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta escrow. 

“Wananchi wa Tanga jiulizeni, hivi msaliti anawezaje kuwang’oa mawaziri wote hao ndani ya kipindi cha miaka mitatu?” alihoji Zitto na kusisitiza kuwa kuna watu wamelenga kutumia hoja hiyo kwa lengo la kumchafua. 
Zitto alisema ni kutokana na kunyanyaswa na kuonewa na viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hivyo aliona njia mbadala ni kutafuta jukwaa lingine la siasa ili aweze kuwatumikia Watanzania.

“Kuanzisha chama kipya siyo kazi nyepesi, lakini kwa sababu tulikuwa na dhamira ya dhati tumeweza kufyeka mapori na sasa tumefanikiwa na leo hii tunakileta kwenu ili mkipokee kwa sababu ACT ni yenu,” Zitto. 

Alisema chama hicho kina mpango wa kuhamasisha ufufuaji wa zao la mkonge mkoani hapa ili lilimwe na wakulima wadogo badala ya wakubwa kwa sababu katika nchi zilizofanikiwa kuleta mapinduzi ya mkonge zimesaidiwa na wakulima wadogo. 

Alisema kupitia ACT atahakikisha hoja yake aliyoiwasilisha bungeni na kupingwa na wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Tanga ya kulifufua zao la mkonge inatekelezwa. 

Mjumbe wa ACT, Seleman Msindi maarufu ‘Afande Sele’ alisema hajajiunga na ACT – Wazalendo kwa sababu ya urafiki wake na Zitto, bali amebaini kuwa ndiyo chama chenye mlengo makini wa kuipeleka nchi kunakostahili mara kitakapofanikiwa kushika dola.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini