KITUO KIPYA CHA DALADALA UBUNGO KUFUNGWA KAMERA ZA CCTV
MANISPAA ya Kinondoni jijini Dar es Salaam itaweka kamera za
CCTV katika kituo kipya cha mabasi Simu 2000 kilichopo Ubungo.
Lengo la hatua ni kurahisisha ukamataji wa wahalifu mbalimbali,
wakiwemo wa miundombinu iliyojengwa.
Mhandisi Mkuu wa manispaa hiyo, Baraka Mkuya alisema hayo
mwishoni mwa wiki wakati akizungumzia kuanza kutumika kwa
kituo hicho.
Alitaka madereva wa daladala na abiria, kuwa waangalifu kwa
matumizi ya miundombinu ya kituo hicho.
Mkuya alisema katika kuangalia usalama wa kituo hicho, Manispaa
imepanga kuweka kamera za CCTV, ambazo zitaweza kuhifadhi
matukio yote yanayotokea kituoni hapo.
“Kamera hizo zitakuwa zikisimamiwa na maofisa wa Polisi na
zitarahisisha upatikanaji wa matukio mbalimbali yanayoweza
kujitokeza kituoni hapo,” alisema Mkuya bila kufafanua zaidi hatua
za uwekwaji wa kamera hizo umefikia wapi.
Aliongeza kuwa ni vyema abiria kujifunza kutumia vyema
miundombinu ya kituo hicho, kilichojengwa kwa Sh bilioni 3.3 ili
kiweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha watu wengi.
Kituo hicho kipya kinachukua nafasi ya kituo cha Ubungo Tanesco,
ambacho kimefungwa ili kutoa nafasi kwa utekelezaji wa mradi wa
ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka katika barabara ya
Morogoro.
NA Lucy Lyatuu