RUSHWA IMESHAMIRI, CHAGUZI ZIJAZO TUTASHUHUDIA MENGI


Jaji Joseph Warioba.
Rushwa ni miongoni mwa vichocheo vikubwa vya umaskini hapa nchini Tanzania.
Siyo kichocheo cha umaskini tu, bali pia ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika nchi ambazo shida hii imeshamiri na kuota mizizi.
Rushwa iliyokithiri katika nchi yoyote, huathiri utawala bora na kushindwa hata kwa nguvu za soko kiuchumi katika nchi husika.Rushwa iliyokithiri siyo tatizo linaloikumba Tanzania peke yake, bali dunia nzima na ni tatizo kubwa sana linalokera jamii, kiasi cha kuhatarisha utulivu na amani katika nchi mbalimbali duniani.
Takwimu zilizotokana na utafiti au tathmini iliyofanywa na taasisi ya kimataifa ya Transparency International, yenye makao yake makuu nchini Ujerumani mwaka 2013, inadhihirisha kuwa rushwa ni tatizo la dunia nzima.
Watanzania watatakiwa waifahamu tafsiri sahihi ya rushwa kwani haishii katika tendo la kutoa au kupokea hongo peke yake ili kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma za kijamii bila bughudha.
Transparency International imeitafsiri rushwa kwa maneno haya yafuatayo: Kwamba ni matumizi mabaya (ya madaraka katika ofisi au taasisi ya umma) kwa manufaa au masilahi binafsi.
Katika tathmini ya viwango vya rushwa kimataifa ya mwaka 2013 , iliyofanywa na taasisi hiyo, Tanzania ilishika nafasi ya 111 miongoni mwa nchi 117 duniani, yaani ni wa sita kutoka mkiani! Aibu kubwa hii!
Tathmini hiyo ilikuwa ni kwa kutumia kiashiria chao kinachoitwa ‘Corruption Perception Index’, ikilinganishwa na nafasi ya 88 miongoni mwa nchi 159 katika tathmini iliyofanyika mwaka 2005.
Hii maana yake ni kwamba rushwa inazidi kukua na kuota mizizi katika nchi yetu na hakika niseme wazi kwamba ni hatari kwa usalama wa nchi yetu, vizazi vya sasa na vijavyo.Rushwa imeingia hata katika mikataba mbalimbali ya nchi, tumeshasikia malalamiko kwenye sekta ya madini, umeme, miundombinu na kadhalika.
Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake alikemea sana ‘mdudu’ rushwa, lakini inaonekana amepuuzwa kwani mianya inaachwa bila kuzibwa.
Tunaelekea kwenye chaguzi mbalimbali kuanzia za viogozi wa serikali ya mitaa au vitongoji na vijiji hadi kwenye udiwani, ubunge na baadaye urais. Ni wakati mwingine wa rushwa kutawala katika jamii na nina hakika tutashuhudia mengi.
Tutashuhudia wagombea wakimwaga fedha na kujifanya ni takrima kwa wapiga kura na makundi yao na nina hakika baada ya chaguzi hizo malalamiko mengi ya utoaji rushwa yatasikika karibu kona mbalimbali za nchi yetu.
Tatizo hili la utoaji na upokeaji rushwa siyo la Tanzania peke yake, bali Afrika Mashariki nzima na duniani kote. Lazima tujitathmini wenyewe. Madhara ya mwenendo huu wa utoaji rushwa kwa vizazi vya sasa upo hivi je, jamii ya vizazi vijavyo itakuwaje?
Hivi sasa kumejengeka kwamba mtu hawezi kupata huduma fulani mpaka atoe rushwa hata kama ni haki yake.Tunaelekea wapi?Hakika, tumejiingiza katika sakata la mambo ambayo hayakubaliki kimaadili duniani kote! Au tumejisahau tulikotoka na hatujui tuendako?
Vijana wetu siku hizi wengi wanadhani na kuamini katika akili zao kuwa bila kutoa rushwa huwezi kufanikiwa katika jambo lolote na hili ndilo linasababisha hata mitihani kuibiwa na kusambaa kwa watahiniwa.
Vijana wa siku hizi wanaamini kuwa ili wapige hatua kimaendeleo basi wapate kazi ambazo mianya ya rushwa ipo nje nje. Wanataka baada ya miaka miwili kazini wawe na nyumba na gari la kisasa kutokana na kula rushwa! Hiyo ndiyo jamii tunayoijenga. Hili ni bomu ambalo lipo mbele yetu.

Ukienda katika hospitali nyingi za umma, rushwa inawekwa mbele ili utibiwe na hata ukitaka haki yako, baadhi ya watendaji watakuomba rushwa.
Vyombo vya kulinda sheria kama mahakama na polisi, baadhi ya watendaji wameonekana kwamba rushwa ni jambo la kawaida. Hata Tume ya Jaji Warioba iliona hili, ikashauri lakini ikapuuzwa, hakuna kilichofanyika kubana mianya hiyo. Tukitaka kupiga hatua kimaendeleo safari hii mtu yeyote ambaye ataomba uongozi wa kuchaguliwa, tukijua kuwa amekuwa akitoa rushwa, atengwe na aogopwe kama ukoma.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …