MCHINA AKAMATWA HUKO PWANI BAADA YA KUMTEKA MWENZAKE, AKUTWA NA RISASI 300
JESHI la Polisi mkoani Pwani
linamshikilia raia wa nchi ya China We Sheng (39) mkazi wa Mbagala
jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumteka nyara Mkurugenzi wa Kiwanda
cha Kutengeneza Viatu vya Plastiki (Yeboyebo), Li Cheng Weng (54) baada
ya kumtishia kwa silaha.Mtuhumiwa huyo alitoa sharti na kumtaka
mlalamikaji atoe fedha kiasi cha dola za Kimarekani 350,000 (sawa na Sh
milioni 584.5) ili amwachie huru.
Akizungumza ofisini kwake mjini Kibaha,
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema tukio hilo
lilitokea Oktoba 19 mwaka huu majira ya saa 4.00 usiku wilayani
Mkuranga.
Kamanda Matei alisema kuwa baada ya
kupekuliwa kwenye gari lake aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za
usajili T 554 BAJ alikutwa na bunduki aina ya Short gun namba 006085010,
risasi 98 na visu viwili.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, Polisi
walikwenda kupekua nyumbani kwa kijana huyo wakakuta nyaraka
zinazoonesha kuwa, amewahi kumiliki risasi 300, hivyo haijafahamika
risasi 202 amezitumia wapi.
Amesema, Ubalozi wa China umewafahamisha polisi kuwa, mtuhumiwa huyo alikuwa akishiriki kufanya uhalifu nchini humo.
Kamanda Matei alisema , polisi
wanawasiliana na wenzao wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ili
kupata taarifa zaidi kuhusu kijana huyo.
Katika tukio lingine, watu watatu
wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamekamatwa wakiwa na bunduki aina ya
Short gun yenye namba 07019302 ikiwa na risasi nane.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mohamed
Kalipa (20) dereva wa Bajaji mkazi wa Mbagala Rangi Tatu, Salum
Shekivui (20) mkazi wa Buza na Seuli Lucas (18) mkazi wa Mbagala Rangi
Tatu jijini Dar es Salaam.
Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 20 mwaka huu majira ya saa 2:30 Mlandizi wilaya ya Kibaha.
“Mbali ya silaha pia walikutwa na fedha
taslimu kiasi cha Shi milioni 6,611,800, vocha mbalimbali za simu zenye
thamani ya Sh milioni 2,185,500 na simu za mkononi sita za aina
mbalimbali ambazo thamani yake bado hazijafahamika,” alisema Kamanda
Matei.
Aidha alisema kuwa watuhumiwa hao
wanadaiwa kuwa walifanya tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha katika
kijiji cha Mbwewe wilaya ya Bagamoyo kwenye duka la Twaha Mbuta, Oktoba
19 saa 1:30 usiku na kupora kiasi cha Sh milioni 30.
“Baada ya kukamatwa walimtaja mtuhumiwa
mwenzao ambaye walikuwa wakishirikiana naye Samwel Joseph mkazi wa
Kongowe, Kibaha ambapo baada ya upekuzi walimkuta na risasi sita za
Short gun ambazo alikuwa akizimiliki bila ya kibali. Hata hivyo
mtuhumiwa huyo alitoroka,” alisema Kamanda Matei.
Katika tukio lingine watu wawili
walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa ng'ombe 61 wenye thamani ya Sh milioni
27.4 mali ya Keke Furaha (37) kwa kutumia silaha aina ya sime.
Alibainisha kuwa tukio hilo limetokea
Oktoba Mosi mwaka huu majira ya saa 5.00 asubuhi eneo la Lulenge kata ya
Ubena wilayani Bagamoyo.
Watuhumiwa katika tukio hilo ni Sadala Lupoto
(25) mkazi wa Kimamba Kilosa na Luseky Sogoyo (25), na juhudi za
kuwatafuta ng'ombe wengine 39 zinaendelea.
Na John Gagarini