POLISI WAJERUHIWA KWA RISASI NA MAJAMBAZI GEITA, WANAHABARI WAZUIWA KUWAPIGA PICHA MAJERUHI HAO


Askari polisi wawili wa kituo cha polisi cha wilaya ya Geita, wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo baada ya kujeruhiwa kwa risasi wakati wa mapambano ya kujibizana na majambazi sita kuzuia uhalifu uliopangwa kufanyika katika kijiji cha Nyakagwe wilayani humo.

Waliojeruhiwa ni Koplo E.18O9 Said na Konstebo G.6212 Hamisi wote wa kitengo cha upelelezi huku jambazi mmoja anayedaiwa ni raia wa Burundi akiuliwa na wananchi baada ya kujeruhiwa kwa risasi na polisi kisha kuchomwa moto baada ya kugundulika amejificha kichakani.

Tukio hilo lililotokea juzi usiku huku mganga wa zamu wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk. George Rweyemera, akisema aliwapokea majeruhi hao na hali zao zinaendelea vizuri. Hamis alijeruhiwa risasi ya mguu wa kulia na Said mkono wa kushoto.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakagwe, Simon Kazungu, alisema wananchi walilipongeza Jeshi la Polisi na askari hao kupambana na majambazi hao na kuzuia uhalifu uliopangwa kutendeka.

Kazungu alisema polisi hao walipelekwa katika kijiji hicho kuongeza nguvu baada ya kuwapo taarifa za kutokea tukio la ujambazi usiku huo na ghafla walivamiwa na kumiminiwa risasi zilizowajeruhiwa kabla ya kujibua mapigo kwa dakika 20 na majambazi kuzidiwa nguvu.

Majambazi hao baada ya kutoroka wawili kati yao wakiwa na bunduki aina ya SMG, walisakwa na wananchi baada ya kuifuata damu iliyokuwa ikimtoka mwenzao na kumkuta akiwa amejibanza na kuanza kushambuliwa hadi kufa kisha kuteketezwa kwa moto.

Kazungu aliongeza kuwa baada ya kumpekua walimkuta na nyaraka zilizomtambulisha ni raia wa Burundi.

Wiki iliyopita watu wengine wenye silaha walivamia kijiji hicho maarufu kwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu na kuiba kiasi Sh.300,000.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea  tukio hilo.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini