Salum Abubakar mchezaji bora Oktoba
Mchezaji wa Azam Salum Abubakar amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba katika Ligi Kuu ya Vodacom, Tanzania Bara. |
Kiungo wa timu ya Azam, Salum Abubakar amechaguliwa kuwa mchezaji bora
wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kutimua vumbi
kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Abubakar ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) aliwashinda wachezaji wengine 20, huku wanne kati ya hao
wakichuana naye kwa karibu.
Wachezaji hao ni Joseph Mahundi wa Coastal Union, Salim Mbonde (Mtibwa
Sugar), Rashid Mandawa (Kagera Sugar) na Najim Magulu wa JKT Ruvu Stars.
Kwa kuibuka mchezaji bora, Abubakar atazawadiwa kikombe na fedha taslimu
sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za
mkononi ya Vodacom.
Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa
mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua
mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na
baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.