MFANYABISHARA BILIONEA WA MADAWA YA KULEVY*A ATIKISA DAR

HII kali! Kukamatwa na polisi kwa mfanyabiashara bilionea jijini Dar, Mharami Mohamed Abadallah ‘Chonji’ (44) (aliyezungushiwa duara) hivi karibuni akidaiwa kukutwa na madawa ya kulevya ‘unga’ aina ya heroin yenye thamani ya shilingi 300,000,000 kumelitikisa Jiji la Dar, Uwazi limefuatalia hatua kwa hatua.
Mfanyabiashara bilionea jijini Dar, Mharami Mohamed Abadallah ‘Chonji’ ((mwenye suti ), akiwa chini ya ulinzi.
Mtikisiko huo umekuja kufuatia maeneo mbalimbali ya jiji kumzungumzia kwa namna mbili, wengine wakifurahia wengine wakisikitika, hasa wanawake wanaoishi maeneo ya Magomeni Kondoa, Dar ambako mfanyabiashara huyo ndiko kwenye makazi yake.
AKUTWA NA SARE ZA JESHI
Tukio lingine liliwatikisa polisi wenyewe kufuatia upekuzi wa kina nyumbani kwake ambapo walimkuta pia na sare mpya za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zinazofanana kwa sehemu kubwa na zile zilizomwingiza Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kwenye mzozo na jeshi hilo.
Sare mpya za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zilizokamatwa nyumbani kwa Billionea huyo.
AKUTWA NA BUTI
Mbali na sare kwa maana ya mavazi, pia mtuhumiwa huyo alikutwa na viatu vya jeshi hilo maarufu kwa jina la buti nazo zikiwa mpya!
BASTOLA NAYO
Katika hali iliyowatia shaka zaidi askari ni pale Mharami alipopekuliwa zaidi na kukutwa na bastola ambayo jeshi la polisi halijaitolea ufafanuzi inaitwaje na ilitengenezwa nchi gani!
Zana zilizokuwa zinatumika na wahalifu nyumbani kwa bilionea huyo kuandaa kete za madawa ya kulevya.
VITU VINGINE
Vitu vingine vilivyokutwa kwa mtuhumiwa huyo ni jiko dogo la gesi na gundi ya plastiki, vyote vinaaminiwa kutumika wakati wa kutengeneza kete za unga tayari kwa kusafirisha.
Mharami, mbali na ishu zote hizo, anadaiwa kumiliki maghorofa mawili, Tandale na Magomeni Kondoa jijini Dar, mabasi na magari manne ya kutembelea mwenyewe.
ALIKAMATWA KAMA KWENYE SINEMA
Mharami alikamatwa Oktoba 21, saa saba usiku nyumbani kwake, Magomeni Kondoa lakini kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo linasemekana kufananishwa na inavyokuwa kwenye sinema za Kimarekani.
Kamanda Godfrey Nzowa akizikagua zana zinazotumika kuandaa kete za madawa ya kulevya.
Inadaiwa kuwa, awali askari zaidi ya 20 kutoka Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania walifika kwenye nyumba hiyo kufuatia kutonywa kuwepo kwa unga na kumbana mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake wanne ndani.Ikadaiwa kuwa, mtuhumiwa na wenzake walijaribu kutoroka walipogongewa mlango na kukataa kufungua.
Chanzo hicho kiliendelea kudai kwamba baada ya Mharami kugoma kufungua mlango polisi walilipua mabomu ya machozi na kupiga risasi hewani ndipo alipokubali kufungua huku wenzake wakiwa wametawanyika kwa kupanda juu ya paa la nyumba ndogo kisha kupanda kwenye jumba la ghorofa tano ambalo analimiliki mtuhumiwa huyo.
Moja ya Ghorofa linadaiwa kuwa ni mali ya bilionea, Mharami Mohamed Abadallah ‘Chonji’
WATU WATOKA NA NGUO ZA KULALIA
Ikazidi kudaiwa kuwa, kufuatia milio ya mabomu na risasi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walitoka kushuhudia wengine wakiwa na nguo za kulalia tu.
ALICHOSEMA MJUMBE, MTENDAJI
Mjumbe wa Nyumba Kumi Shina Na. 2, Mwanamtama Sasamalo alipohojiwa na Uwazi alikiri kutokea kwa tukio hilo la kamatakamata ya askari kwa Mharami na wenzake.
Baadhi ya wahalifu wakichukuliwa kutoka Mahakama ya Kisutu.
“Ilikuwa kama saa saba usiku, polisi walinigongea nyumbani kwangu wakasema wanataka kumkamata mhalifu, tukafuatana hadi nyumbani kwa Mharami. Niliwakuta polisi wengine wakiwa na silaha wameizingira nyumba yake, nilichokishuhudia ni ungaunga ukiwa umesambaa chini, wahusika walikamatwa na kufuatana na askari,” alisema mjumbe huyo.
Naye Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Makanya, Kata ya Ndugubi, Alex Mwisongo alipoulizwa alisema tukio hilo lipo, akaongeza kuwa vijana wengi wamekuwa mateja katika mtaa wake na wameathiriwa na unga ambao hajajua unakotoka.
Bilionea Mharami akiwa na wahalifu wenzake wanne chini ya ulinzi mkali ndani ya Mahakama ya Kisutu.
KAMANDA NZOWA SASA
Naye Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Godfrey Nzowa alipoulizwa na waandishi wetu ofisini kwake alisema Mharami alishawahi kukamatwa mwaka 2009 kwa kuhusishwa na madawa ya kulevya ambapo alikuwa chini ya uangalizi wa polisi na mahakama.


Aliwataja waliokamatwa naye safari hii kuwa ni Rehani Mursal (45), mkazi wa Mburahati (Dar), Abdul Abdallah (37), mkazi wa Mbezi Shamba (Dar), Tanaka Mwakasaburi (35), mkazi wa Magomeni- Makanya (Dar) na Maliki Zuberi (29), mkazi wa Magomeni Mwembechai (Dar).
Mharami na wenzake wakipandishwa kizimbani kwenda kusomewa mashitaka.
Watuhumiwa hao wote walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar, wiki iliyopita chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi na askari magereza mbele ya Hakimu Janeth Kaluyenda na walipelekwa mahabusu ya Gereza la Keko, wanatarajiwa kurudi mahakamani Novemba 6, mwaka huu.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini