Tatianala umeme jijini Dar kuendelea hadi Novemba 2, 2014
Tatizo la
kukatika kwa umeme litaendelea hadi Jumapili Novemba 2, 2014 ikiwa
matengenezo ya mitambo ya uzalishaji umeme ya Tegeta na Ubungo, Dar es
Salaam yatakamilika kwa wakati, FikraPevu imefahamishwa.
Tatizo la kukatika kwa umeme limeenza kujitokeza kwa siku kadhaa sasa na taarifa za ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zinaeleza kwamba kuna matengenezo ya kawaida (maintenance) kwa mitambo ya Tegeta na Ubungo.
FikraPevu imebaini
kwamba mbali ya matengenezo ya mitambo hiyo, kuna taarifa kwamba
wazalishaji wa gesi nao wanafanyia matengenezo ya mfumo wao na kupunguza
utoaji wa gesi inayopelekwa kwenye mitambo ya Tanesco kipindi ambacho
shirika hilo limemaliza akiba ya nishati hiyo.
Kumekuwa na
utata kuhusiana na tatizo la umeme katika baadhi ya maeneo mbalimbali ya
nchi likiwamo jiji la Dar es Salaam kutokana na wahudumu wa Tanesco
kudaiwa kuudanganya umma wanapopigiwa simu kwamba kuna hitilafu katika
eneo husika.
Utafiti wa FikraPevu umebaini
kwamba taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwa wateja wa maeneo yote bila
kujali utofauti wa kijiografia. Mfano jibu la “Mafundi wetu
wanafuatilia, kuna tatizo limetokea hapo mtaani kwenu,” hutolewa kwa
wateja wa Ilala, Kariakoo, Temeke, Kinondoni, Kijitonyama, Tabata,
Kimara, Sinza na Upanga.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimeijulisha FikraPevu kwamba
kuna wasiwasi wa kuwapo hujuma ama uzembe na wananchi wamehoji
“Inakuwaje ‘maintanence’ ya mitambo na mifumo ya uzalishaji umeme
ikafanyika kwa wakati mmoja na katika kipindi ambacho akiba ya gesi
imekwisha?”.
FikraPevu imejulishwa
pia kwamba hivi karibuni Tanesco ilisitisha ununuzi wa umeme kutoka kwa
mzalishaji binafsi kutokana shirika hilo kuwa na umeme wa kutosha
kutoka katika mitambo yake inayoendeshwa na maji.