MFANYABIASHARA AJIUA KWA KUJIPIGA RISASI KWENYE BAA JIJINI ARUSHA
MFANYABIASHARA wa Arusha anayemiliki kampuni ya Tanzania
Bush Camp yenye kambi za watalii katika hifadhi za Serengeti
mkoani Mara na Manyara iliyopo katika mikoa ya Arusha na
Manyara, Timoth Mroki (36) amejiua kwa kujipiga risasi tatu kifuani
akiwa katika baa maarufu ya Arusha Raha iliyopo eneo la Shams,
jijini hapa.
Kisa cha kujiua kwake kimetajwa ni kusababisha ajali, baada ya
kuligonga gari lingine katika eneo la Mbauda wakati akitoka katika
makazi yake yaliyopo eneo la Kwa Mrombo, jijini hapa.
Alifikwa na mauti katika tukio lililotokea kati ya saa 1:30 na saa
2:00 usiku, ndani ya baa hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mroki alifika katika baa
hiyo baada ya kufanikiwa kuwatishia kwa risasi waendesha
bodaboda waliokuwa wamemzingira katika eneo la ajali na kisha
kuondoka kwa kasi kwa gari lake aina ya Nissan Navara.
“Alipiga risasi mbili hewani waliokuwa wamemzunguka wakanywea,
akatumia mwanya huo kukimbia na moja kwa moja akafika Arusha
Raha pengine kwa lengo la kujificha, na hapo akaanza kunywa…
“Ingawa inaonekana alikotoka alikunywa kidogo, alipofika Arusha
Raha alikunywa haraka pombe mbili kali aina ya Valuu (Valeur) na
wakati anamalizia ya tatu, akajikuta anazingirwa tena na wale
waendesha bodaboda,” anasema mtoa habari huyo na kuongeza
kuwa, baada ya kufyatua tena risasi mbili nyingine hewani, lakini
bila ya dalili ya watu hao kutishika, ndipo akaamua kujimiminia
risasi.
Habari zaidi zinasema wakati anazingirwa, naye akijihami kwa risasi
wasamaria wakiwa katika harakati za kupiga simu Polisi
walishtukia wakiingia katika eneo la tukio lakini tayari Mroki
alikuwa ameshajitoa uhai baada ya kujimiminia risasi kifuani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatusa Sabas
hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, ingawa Ofisi ya Mkuu wa
Upelelezi ya wilaya ya Arusha imekiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini
chanzo chetu kikikataa kutajwa jina gazetini kwa kuwa si wasemaji
wa matukio ya polisi mkoani Arusha.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi
maiti cha Hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Na John Mhala, Arusha