CHADEMA IRINGA WADAI POLISI NAO WANAFANYA MAANDAMANO BILA KUJIJUA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Iringa Mjini, jana kimeshindwa kufanya maandamano ya amani kama ilivyotangazwa kwa kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wake, Frank Nyalusi, kuzuiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa.
 
Nyalusi ambaye ni diwani wa Mivinjeni, alisema kuwa maandamano yanayofanyika mkoani hapa licha ya zuio la jeshi la polisi ni ya kisasa zaidi, kwa kuwa yanawahusu askari wenyewe kuandamana kwa kuweka ulinzi, hivyo kuandamana wao pasipo kujua.
Alisema jeshi la polisi linaandamana nchi nzima kwa kuwakea ulinzi pasipo kujua kuwa, hata wananchi wanaandamana kisasa kwa kuwafuata wao kila wanapokwenda kwa lengo la kujua kama wanachama wa CHADEMA na wafuasi wake wanaandamana.
Alisema walitoa taarifa kwa jeshi hilo siku mbili zilizopita wakielezea nia yao ya kufanya maandamano hayo, ikiwa ni kuitikia wito uliotangazwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe wa kufanya maandamano ya amani yasio na ukomo yenye lengo la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Alisema pamoja na jeshi hilo kuwazuia kufanya maandamano hayo, jana hiyo hiyo waliruhusiwa kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wenye wafanyabiashara ndogondogo (Machinga), maarufu kama Magari Mabovu Kata ya Kitanzini.
Wakati CHADEMA wakidai kudhibitiwa kufanya maandamano hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema jeshi hilo halijapokea barua yoyote kutoka chama hicho inayoonesha wameomba kufanya maandamano hayo.
Akitoa ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema; “Nchi hii kama zilivyo nchi nyingine inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni.”
Alisema watanzania bila kujali wanatoka kundi gani ni lazima wafanye mambo wanayotaka kwa kuzingatia sheria, vinginevyo mkono wa sheria utawafukuzia.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini