WATOTO WADAIWA KUMUUA BABA YAO KWA KUMPIGA FIMBO WAKIMTUHUMU KUUZA CHAKULA CHA FAMILIA


JESHI la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watoto watatu, kwa tuhuma za kumpiga fimbo kichwani baba yao mzazi na kumsababishia kifo.
 
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Gilles Muroto, alisema tukio hilo ni la mwezi Septemba 15, mwaka huu katika Kijiji cha Mkunyu Kata ya Kikukuru Tarafa ya Mabira wilayani Kyerwa.
 
Alisema siku ya tukio, watuhumiwa hao, ambao hakuwataja majina yao kutokana na umri wao kuwa chini ya miaka 18, walimuua baba yao, Henry Siliakus (62) kwa kumchapa fimbo kichwani akiwa nyumbani kwake hadi akapoteza uhai wake.

 
Muroto alisema watoto hao, mmoja wao ana umri wa miaka 17, anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mkunyu.

 
Mwingine ana umri wa miaka 13, anasoma darasa la nne. Mwingine ana umri wa miaka 11, anasoma darasa la tatu. Wote wawili wanasoma katika Shule ya Msingi Mkunyu.

 
Kamanda alisema sababu ya awali ya mtafaruku huo, uliosababisha kifo ni ugomvi wa baba na watoto wake, kwa kile kinachodaiwa baba yao kuwa na tabia ya kuuza chakula cha familia na kuwaacha wakitaabika na njaa.

 
Kamanda alisema jeshi hilo, bado linaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na litawafikisha mahakamani watoto hao pale taratibu za kisheria zitakapokamilika.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini