KWA NINI WATU WENGI HAWAFANIKIWI MAISHANI?- 8

NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu unaendelea vizuri na kazi ya kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo kupitia ujasiriamali. Mada tunayoendelea kuijadili ni sababu zinazofanya watu wengi washindwe kufanikiwa.
Wiki iliyopita, niliishia kueleza kwamba watu wengi hawafanikiwi kwa sababu hawawezi kuwa mabahili katika matumizi ya pesa wanazozipata. Niliishia kukupa mfano wa jinsi mimi na dada yangu tulivyokuwa na hulka tofauti za matumizi ya pesa tulipokwenda kwenye mashindano ya Umiseta mjini Songea. 
Kabla sijaendelea mbele, ningependa kumalizia mfano huo:


Mzee wetu alitupatia Sh. 5,000 kila mtu kama ‘pocket money’ na pesa ya kutumia njiani wakati wa safari. Kwa wakati huo ilikuwa ni pesa nyingi sana kwa mwanafunzi. Pengine kwa nyakati hizi ingekuwa ni zaidi ya shilingi laki moja.
Cha kushangaza ni kwamba, mara baada ya kufika tu Songea ambako tulipaswa kukaa kwa wiki moja kamili mimi nilianza kutumia ile pesa hovyohovyo kama vile kununua chips kuku,  soda za mara kwa mara pamoja na marafiki, kwenda muziki n.k.
Baada ya siku mbili tu, nikawa nimeishiwa kabisa. Sasa kumbuka mwaka 1992 shilingi 5000 ni pesa nyingi sana. Baada ya hapo nikawa sina ujanja zaidi ya kwenda kucheki na dada Mary kama yeye alikuwa bado na kiasi ili anikopeshe.
Kilichonishangaza ni kwamba Mary alikuwa hajatumia hata senti moja katika ile 5000/- yake! Wow! Hilo jambo lilinishangaza kupita maelezo ya kawaida.  Hivyo ilikuwa wazi kwamba  mimi nilikuwa mfujaji wakati dada yangu alikuwa mtunzaji. Je, wewe ni mfujaji au mtunzaji?
Wakati mwingine ambapo somo hili lilijirudia vizuri sana, ilikuja kuwa takriban miaka 13 baadaye. Mwaka 2005 nikiwa kwenye ajira zangu za mwisho mwisho kabla sijajiajiri, nilikuwa nafanya kazi kama ofisa mauzo wa Apsi Business Manager jijini Dar es Salaam. Kampuni ilikuwa ndogo ya wastani yenye watu kama 10 hivi pamoja na wakurugenzi wake.
Lakini kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa mesenja pale ofisini kwa jina la Jose. Mara kwa mara, baada ya sisi sote wafanyakazi (kasoro wakurugenzi kuishiwa) tulikuwa tunakimbilia kwa Jose kumuazima pesa. Pamoja na kwamba Jose alikuwa na mshahara mdogo kuliko wote, lakini ndiye aliyekuwa na udhibiti mkubwa wa pesa kuliko sisi maofisa wengine wote! Ni ajabu sana.
Hivyo, haijalishi unalipwa kiasi gani cha pesa kila siku, wiki au mwezi, inajalisha unaweza kutunza kiasi gani cha pesa hiyo. Kwa hivyo weka malengo ya kudhibiti pesa yako leo ili uanze kuchangisha kwa ajili ya mtaji wako wa biashara au kwa ajili ya mambo ya msingi zaidi maishani.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini