Mdee amfunika Magufuli

Mbunge wa Kawe kwa tiketi ya Chadema akiongea na wakazi wa Chato mkoani Geita hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), Halima Mdee, amebomoa ngome ya mbunge wa Chato, Dk. John Magufuli kwa kuzoa wanachama zaidi ya 300 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa katika ziara yake wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Dk. Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, amejizolea umaarufu mkubwa nchini kiasi cha kujijengea taswira kwamba anaungwa mkono jimboni kwake, ambapo sasa kwa pigo hilo la Mdee, atapaswa kujipanga upya.
Akiendelea na ziara yake ya Kanda ya Ziwa ya kuimarisha chama na kuhamasisha wananchi waikatae Katiba mpya inayopendekezwa, Mdee  aliwapokea wanachama hao wa CCM na kuwakabidhi kadi za CHADEMA kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika juzi katika viwanja vya stendi ya zamani.
Wanachama hao walieleza kuwa sababu iliyowasukuma kukihama chama hicho ni kutokana na kuchoshwa na kauli za kejeli za mbunge wao, Dk. Magufuli kila wanapomhoji kuhusu utekelezaji wa ahadi zake.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Christopha Masanja alisema kuwa wanakabiliwa na kero nyingi ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama licha ya kuwa karibu na ziwa Victoria, lakini kila wanapojaribu kumweleza mbunge wao, huishia kuwapa kauli za kejeli.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi, Mdee alisema kuwa serikali ya CCM imekuwa haiwathamini wananchi wake ndio maana imeshindwa kutoa kipaumbele kinachostahili katika kutatua kero zao na badala yake kuelekaza fedha nyingi kwenye mambo yasiyo na msingi.
Alisema kuwa sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa Watanzania zaidi ya aslimia 80 imetengewa kiasi kidogo cha fedha kwenye bajeti ya mwaka huu
ya sh. bilioni 42  huku safari za rais zikitengewa sh. bilioni 50.
Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe, aliwataka wananchi wa Chato kufanya mabadiliko na kuondoa uteja kwa CCM akisema kuwa licha ya kuwapa kura tokea nchi ipate uhuru lakini wameshindwa kuwatatulia kero zao.
Aliwataka kutorudia makosa hayo kwenye chaguzi zijazo badala yake wahakikishe kwenye ngazi zote za uwakilishi wanachagua wagombea watakaosimamishwa na CHADEMA.
Chanzo: Tanzania Daima.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini