Kuhusu maandamano ya wafanyakazi wa Tanzanite One



WACHIMBAJI wadogo wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanatarajia kuandamana hadi kwa mkuu wa mkoa huo, wakipinga kusimamishwa kazi migodi yao 19 inayopakana na TanzaniteOne.


Wachimbaji hao wanatarajia kuandamana kwa amani mapema mwezi ujao na watamuandikia barua mkuu wa mkoa huo Dk Joel Bendera ili ayapokee maandamano hayo wakipinga kunyanyaswa na kusimamishwa migodi yao 19.


Mmoja kati ya wachimbaji hao Charles Mlay akizungumza juzi kwenye mkutano wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite Marema, alisema wachimbaji wamekuwa wananyimwa haki zao bila sababu ya msingi.


“Hakuna mtu aliye juu ya sheria kila wakati wachimbaji wadogo wananyanyasika kwa kunyimwa haki zao wakati wanachimba kihalali hivyo ni bora kufanya maandamano ya amani yatakayoeleza hisia zetu,” alisema Mlay.


Makamu Mwenyekiti wa Marema Wariamangi Sumari alisema maandamano hayo ya amani yatajumuisha wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na wakazi wote wa Mirerani kwani maisha yao yanategemea madini ya Tanzanite.


“Maandamano hayo yatakuwa ya halali kabisa kwani tutaomba kibali kwa mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) na kumtaarifu mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa aje hapa Mirerani kwa ajili ya kupokea maandamano hayo,” alisema Sumari.


Omary Mandari alisema kitendo cha migodi hiyo 19 kusimamishwa kufanya kazi kimewaathiri watu wengi kiuchumi, kwani familia nyingi za wachimbaji hao zinategemea kuishi ila kutokana na hali hiyo, sasa wanaishi kwa wakati mgumu.


“Tutaandamana kwa amani kuanzia shamba la Maro na kuzungukia kwenye baadhi ya barabara za Mirerani hadi getini mnadani, kwa lengo la kuonyesha ulimwengu kuwa tunapinga migodi yetu 19 kusimamishwa,” alisema Mandari.


Naye, katibu wa Marema Abubakari Madiwa alisema azimio hilo la kuandamana kwa wachimbaji hao wadogo linaandaliwa ipasavyo ikiwemo kamati ndogo itakayoratibu mpango wote hadi kufanikisha maandamano hayo ya amani.


Zephania Joseph alisema haki ya wachimbaji wadogo haiombwi inadaiwa, hivyo huu ni wakati muafaka wa kuungana kwa wachimbaji hao kufanya maandamano ya amani ili kufikisha kilio cha kwa migodi yao 19 kusimamishwa.

ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini