Wizara Afya yatoa taarifa ya hali ya Kipindupindu nchini




Waziri Ummy Mwalimu alizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na hali ya kipindupindu nchini ambapo hadi sasa ni mikoa 21 ya Tanzania Bara imeathirika. Jumla ya watu 12,222 wameugua kipindupindu na kati yao watu 196 wameshafariki.


Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wakimfuatilia waziri huyo(hayupo pichani) alipokuwa akitoa taarifa hiyo.Hata hivyo Waziri Ummy ameagiza kila wiki (jumatatu) wizara yake kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya kipindupindi kila mkoa.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiongea na waandishi wa habari.


Waziri Ummy amesema, kwa taarifa ya hadi kufikia leo tarehe 28 Desemba, 2015 kumekuwa na wagonjwa wapya 76 na kufanya jumla ya wagonjwa wanaoendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma kwenye mikoa iliyoathirika kuwa 115 na kifo kimoja kipya (1). K ulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (Tanzania), Dkt.Rufaro Chatora.


Waziri Ummy mwalimu akisikiliza maswali toka kwa waandishi wa habari, kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo John Michael. Aidha amezitaja Halmashauri zinazoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Morogoro Vijijini(12), Iramba (7), Simanjiro(7), Arusha Mjini(6) pamoja na Uvinza (4).


TAMKO LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU, WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, KUHUSU HALI YA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI 28 DESEMBA 2015

Ninapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu ulioanza tarehe 15 Agosti, 2015 katika mkoa wa Dar es Salaam na kusambaa kwa kasi katika Mikoa mingine 21 ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na Pwani, Morogoro, Iringa, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Geita, Mara, Manyara, Arusha, Shinyanga, Tabora, Singida, Tanga, Lindi, Rukwa, Kagera, Katavi, Mbeya na Mwanza na Simiyu.

Tangu ugonjwa huu uanze, jumla ya watu 12,222 wameugua Kipindupindu, na kati yao jumla ya watu 196 wameshafariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na asilimia 1.6 ya waliougua. Mkoa ambao umekuwa na wagonjwa wengi tangu mlipuko uanze ni Dar es Salaam 4,652 (asilimia 38 ya wagonjwa wote) ukifuatiwa na Tanga 1,470 (asilimia12), Singida 1016 (asilimia 8) Mwanza 909 (asilimia 7), Mara 804 (asilimia 7) na Arusha 756 (asilimia 7).

Katika kipindi cha wiki mbili za kwanza za mwezi Desemba 2015, mikoa ya Mbeya (Kyela), Arusha (Arusha Mjini) na Mara (Musoma Vijijini) ilikuwa inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wapya wengi zaidi wa Kipindupindu. Kadhalika, mikoa ya Kigoma, Rukwa na Lindi ilianza kuripoti upya ugonjwa huu katika kipindi tajwa hapo juu. Aidha, Mikoa ya Tanga na Singida, ambayo hapo nyuma ilipata nafuu, sasa imeanza tena kuripoti ugonjwa huu.

Hata hivyo, kasi ya ongezeko la ugonjwa imepungua katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Mbeya na Dar-es-Salaam kutokana na juhudi zinazofanywa na wadau ambao kwa pamoja, wameshirikiana kudhibiti ugonjwa huu kwa karibu zaidi. Aidha, mikoa ya Iringa na Kilimanjaro imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu ambapo hakuna mgonjwa mpya kwa zaidi ya siku 30 zilizopita.

Kwa mujibu wa taarifa ya tarehe 28 Desemba kumekuwa na wagonjwa wapya 76 na kufanya jumla ya wagonjwa wanaoendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa yote iliyoathirika kuwa 115 na kifo kipya kimoja (1). Halmashauri inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Morogoro Vijijini (12), Iramba (7), Simanjiro (7), Arusha Mjini (6) na Uvinza (4).

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Sekta nyingine husika, wadau wa maendeleo na wadau wengine inaendelea kukabiliana na ugonjwa huu kwa njia mbalimbali. Ofisi ya Rais iliitisha kikao cha pamoja katika ngazi ya Mawaziri na pia iliitisha kikao kingine kwa kushirikisha Wizara yangu, TAMISEMI, Wizara ya Maji, DAWASCO, DAWASA, Wizara ya Elimu na Sekretariat ya Mkoa wa Dar-es-Salaam. Lengo lilikuwa ni kupanga mikakati jumuishi na ya haraka itakayoweza kufanikisha udhibiti wa ugonjwa huu.

Kutokana na mwenendo wa mlipuko wa kipindupindu nchini, naendelea kusisitiza kuwa, maagizo niliyoyatoa tarehe 16 Desemba 2015 yazingatiwe na wananchi ili kudhibiti ugonjwa na kuokoa vifo vinavyotokana na ugonjwa huu. Maagizo haya ni pamoja na kunywa maji yaliyo safi na salama, kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka kwa kabla na baada ya kula, baada ya kutoka chooni, baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia, baada ya kumhudumia mgonjwa.



Aidha, ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, mabwawa na ziwani.

Pia nasisitiza tena kuwa ni marufuku kuuza matunda yaliyokatwa na vyakula barabarani katika mazingira yasiyo safi na salama.

Aidha, maagizo niliyoyatoa hapo awali kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji ambao ni Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Afya yaendelee kutekelezwa na kutolewa taarifa kwa wakati.

Na kutokana na hili, nimeagiza kuandaliwa kwa taarifa ya mlipuko kwa kila wiki ili kupata hali halisi, na kila jumatatu wizara itatoa taarifa ya kila wiki ya ugonjwa.

Kama nilivyosema hapo awali, kwa kuwa ugonjwa huu bado unaendelea kusambaa, mikoa ambayo bado haijaathirika ichukue hatua za tahadhari za kuzuia ili isipate mgonjwa yeyote wa Kipindupindu. Wizara itaendelea kufanya tathmini ya hatua zinazochukuliwa ili hatua stahiki zichukuliwe kuudhibti na kuutokomeza ugonjwa huu.


ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini