Waziri mkuu aguswa na ujumbe wa mabango....atoa maagizo huko Kigoma


Na Emmanuel Senny, Kigoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Bandari mkoani Kigoma (TPA) kupitia upya zoezi linalolalamikiwa na wananchi kuhusu fidia.


Akizungumza na wananchi baada ya kufungua soko jipya la Samaki lililoko kata ya Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Waziri Majaliwa alisema kuwa, katika kutekeleza miradi ya maendeleo kuna wananchi walioathirika baada ya kutakiwa kupisha miradi hiyo.


Alisema kuwa, kisheria wananchi wote wanaohamishwa katika maeneo yao hutakiwa kulipwa fidia ambapo katika mradi wa upanuzi wa bandari ya Kigoma ambao ulipeleka kuhamishwa kwa baadhi ya wananchi wa Kibirizi, wapo waliolipwa fidia na wengine hawakulipwa huku wengine wakilalamikia kulipwa fidia ndogo.


“Nimeona wananchi wakiwa na mabango wakinihitaji niwasaidie katika suala la fidia na wanadai haki haikutendeka pia hata Mbunge wao Zitto Kabwe amegusia malalamiko ya wananchi ” alisema Waziri Majaliwa.


Aidha Majaliwa alisema kuwa, Mamlaka ya bandari inatakiwa kupitia upya suala la fidia kwa wananchi wa kibirizi kwa kukagua kila eneo la mtu na thamani ya pesa aliyolipwa pia kuwalipa wale ambao hawakulipwa.


“Suala la hili litafanyika mara moja mara baada ya mimi kuonana na viongozi wa mamlaka ya bandari na nitahitaji kama kuna mtu alilipwa fidia ndogo basi aongezwe kulingana na thamani ya eneo lake na kwa wale ambao hawajalipwa kama maeneo yao yako kwenye mradi basi walipwe mara moja ” alisisitiza Waziri Majaliwa.


Hata hivyo Waziri Majaliwa alisema kuwa, suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni endeleavu ambapo kwa Kigoma kuna mradi wa upanuzi wa bandari na ujenzi wa bandari ya nchi kavu na miradi hii yote inagusa maeneo ya wananchi hivyo serikali inatakiwa kulipa fidia stahiki kwa kila mwananchi wa eneo husika.


Awali Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri Majaliwa kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu suala la fidia ambalo linaonekana kuwa kero kutokana na wengi kulipwa fidia ndogo huku wengine kutokulipwa kabisa.


“Kama unavyoona Mheshimiwa Waziri Mkuu mabango ya wananchi wanaomba uwasaidie katika suala hili maana kama miradi hii ni kwa lengo la kuleta maendeleo basi wananchi waiunge mkono ila hawawezi kuunga mkono kama mamlaka husika haziwalipi fidia zao kama kama thamani ya maeneo yao ilivyo ” alisema Kabwe.

ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini