Mahakama kuu yamfutia kesi Waziri Mwakyembe


Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imeitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Abraham Mwanyamaki, dhidi ya Mbunge wa Kyela na Waziri wa Katiba na Sheria, Dokta Harrison Mwakyembe.


Mahakama imefikia hatua hiyo baada ya Mwanyamaki kushindwa kulipa ada ya gharama za uendeshaji wa kesi hiyo shilingi Milioni Tatu katika muda wa Siku 14 uliowekwa kisheria.


Baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2015, Jumla ya kesi Sita zimefunguliwa kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, kupinga matokeo ya uchaguzi, Tano ni za waliokuwa wagombea wa CHADEMA dhidi ya walioshinda kutoka CCM na Moja ni ya Mgombea wa CCM dhidi ya aliyeshinda kwa CHADEMA.


Hata hivyo, Jaji wa mahakama hiyo, Atuganile Ngwala, ameitupilia mbali kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea wa CHADEMA, katika jimbo la Kyela, Abraham Mwanyamaki, dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Katiba na Sheria, Dokta Harrison Mwakyembe, baada ya Mwanyamaki kushindwa kulipa ada ya gharama za uendeshaji wa kesi hiyo ambazo ni shilingi Milioni Tatu katika muda uliowekwa wa siku 14 kuanzia Disemba 10 hadi 23 mwaka huu.


Mbali na kuifuta kesi hiyo, Jaji Ngwala, pia amemuagiza Mwanyamaki, kulipa gharama zilizojitokeza kwa upande wa Mlalamikiwa Dokta Mwakyembe na jopo la Wanasheria wake kutokana na matumizi waliyoyafanya katika kufuatilia shauri hilo hadi linatupiliwa mbali na mahakama hiyo.


Licha ya kulifuta shauri hilo, mahakama hiyo imeridhika kuwa kesi nyingine Tano zimekidhi vigezo vya kisheria hivyo zitatajwa mahakamani hapo Januari Saba mwakani ili kuendelea na taratibu za kisheria za uendeshaji wa kesi za aina hiyo.


Kesi hizo ni iliyofunguliwa na Kada wa CCM Dokta Lucas Siyame dhidi ya Mbunge wa Momba kupitia CHADEMA, David Silinde, kesi ya John Mwambigija wa CHADEMA dhidi ya Mbunge wa Rungwe kwa tiketi ya CCM, Saul Amon na shauri la Liberatus Mwang’ombe wa CHADEMA dhidi ya Mbunge wa Mbarali, Haroun PirMohammed wa CCM.


Kesi nyingine ni ya Fanuel Mkisi wa CHADEMA akipinga ushindi wa Mbunge wa Vwawa kupitia CCM, Japhet Hasunga na shuari lililofunguliwa na Adam Zela wa CHADEMA dhidi ya Mbunge wa Mbeya Vijijini kwa tiketi ya CCM, Oran Njeza.


Mbeya ina majimbo 13 ya uchaguzi, kutokana na kesi hizo Wabunge wa majimbo Manane ambayo ni Mbeya Mjini, Lupa, Songwe, Tunduma, Mbozi, Ileje, Busokelo na Kyela ndiyo wenye uhakika wa kuendelea na shughuli zao za ubunge bila ya kutikiswa na kesi mahakamani.


ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini