Jeshi la Polisi mkoani Singida lamshikilia mtu anayedhaniwa kuwa jambazi sugu


Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP.Thobias Sedoyeka.

Na Nathaniel Limu, Singida

Jeshi la polisi mkoani Singida,limefanikiwa kukamata mkulima na mkazi wa Kibaoni Iddy Issah (33), anayedhaniwa kuwa ni jambazi sugu baada ya kulipiga risasi moja mguu wake wa kulia, wakati alipojaribu kutoroka.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Singida, ACP Simon Haule,alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa Januari tatu mwaka huu saa 7.20 usiku katika baa ya Leaders iliyopo kata ya Kindai tarafa ya Unyakumi manispaa ya Singida.

Alisema siku ya tukio askari polisi walipokuwa kwenye doria katika mitaa ya kata ya Kindai, walipata taarifa za kiintelijensia kuwa mtuhumiwa yupo baa ya Leaders maeneo ya Kibaoni.

“Baada ya polisi hao kupata taarifa hizo,walifika haraka kwenye baa hiyo na kujaribu kumkamata mtuhumiwa.Lakini alipambana nao huku akitaka kumnyang’anya silaha mmoja wa askari polisi hao,hata hivyo,hakuweza kufanikiwa”,alisema Haule.

Kaimu kamanda huyo,alisema baada mtuhumiwa kushindwa kupora silaha, alifanikiwa kukimbia akitaka kutoroka ndipo askari mmoja alifyetua risasi mbili hewani, ili kumwongofya aweze kusimama.Hakuweza kusimama,kitendo kilichomlazimisha askari kumjeruhi mguu wa kulia.

Kuhusu tuhuma zinazomkabili mtuhumiwa, Haule alisema amefunguliwa kesi SI/IR/4412/2015 ya kuvunja nyumba usiku na kumwimbia raia wa kigeni kutoka China, shilingi 17,442,000.

“Mwaka jana pia alifunguliwa kesi no.SI/1R/4722/2015 ya kuvunja nyumba usiku na kuiba shilingi 200,000 mali ya raia wa kigeni kutoka Korea. Ana kesi nyingine no.SI/1R/4723/2015 ya kuvunja nyumba usiku na kuiba fedha na simu vyote vikiwa na thamani shilingi 3,101,000.Makosa hayo yote yanaangukia chini ya kifungu cha sheria namba 294 (2) na 296 (a) vya kanuni ya adhabu”, alifafanua.

Alisema kwa sasa mtuhumiwa Iddy amelazwa wodi namba tatu katika hospitali ya mkoa mjini hapa chini ya ulinzi mkali, na hali yake inaendelea vizuri.

Haule alisema baada ya upelelezi zaidi kukamilika,mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini