Mbunge wa Kinondoni Mhe. Maulid Mtulya Awasilisha Pingamizi Mahakamani kuhusu Zoezi la Bomoabomoa Katika Jimbo Lake
Mbunge wa jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia amewasilisha mahakamani shauri la kupinga zoezi la ‘bomoabomoa’ linaloendelea jijini Dar es Salaam.
Shauri hilo lenye uwakilishi wa wananchi nane linatarajiwa kusikilizwa katika mahakama Kuu kitengo cha Ardhi, leo (Januari 4).
Kwa mujibu wa Mtulia, Shauri hilo lilifunguliwa mahakamani hapo Desemba 22 na kupata faili rasmi Desemba 28 mwaka jana. Katika shauri hilo, walalamikaji wanaiomba mahakama kuamuru usitishwaji wa zoezi la bomoabomoa ili kuwapa muda zaidi wananchi kujiandaa kupisha maeneo hayo lakini pia kuwatafutia makazi mbadala.
“Kimsingi tunachokiomba sisi ni kwamba suala la ubomoaji kwanza lianze na mazungumzo kwamba kila mtu alipwe haki yake ndipo ubomoaji ufanywe. Na wananchi wa mabondeni wasitolewe muhanga. Na ninashukuru kwa sababu serikali imesema inasimamia sheria basi naamini kwa kwenda mahakamani basi sheria itafuata mkondo wake,”alisema Tulia.
Shauri lililofunguliwa mahakama kuu ni shauri dogo linalofahamika kama ‘Miscellaneous land application’ namba 822 ya mwaka 2015.
Mtulia ameeleza kuwa kuna watu zoezi hilo halijawatendeea haki. Alitoa mfano kuwa viwanja 200 vilitolewa na serikali kwa ajili ya wananchi waliobomolewa, lakini nyumba 800 zilibomolewa. Hivyo, watu 600 waliobomolewa bado hawajapewa viwanja.