SOMA HII KAULI YA WAZIRI MKUU MAJALIWA BAADA YA KUKAGUA HALI YA CHAKULA MKOANI RUVUMA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU AFURAHISHWA NA HALI YA CHAKULA MKOANI RUVUMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefurahishwa na hali ya chakula mkoani Ruvuma, ikiwa kati ya mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi nchini.
Akizungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali jana jioni (Jumapili, Januari 3, 2016) katika ukumbi uliopo Ikulu ndogo Songea, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa kuhakikisha kuna upatikanaji wa masoko kwa mazao mbalimbali pamoja na kuendelea kutoa msukumo kwa wananchi.
Pia, ameupongeza uongozi wa mkoa huo kwa kutoa msukumo kwa wananchi na kufanyakazi, na kusema ni jambo linalosaidia kupanda kwa pato la mtu mmoja mmoja, hata hivyo hakusita kuwashukuru kwa mapokezi makubwa aliyopata.
“Nawapongeza sana wana Ruvuma kwa kuongeza pato la ndani kutoka shilingi 654,227, hadi kufikia shilingi 1,800,000 kwa kipindi cha mika 4 tuendelee kujiweka vizuri kwa kuongeza pato la mtu mmoja mmoja”alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa pia amesisitiza kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yote yenye mabonde ili wakulima waweze kuvuna bila kutegemea sana kipindi cha masika. Amesema ni lazima kuimarisha huduma muhimu na kusisitiza matumizi mazuri ya fedha zinazopatikana katika mazao hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu amesema zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Ruvuma hutegemea kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara yakiwemo mahindi, mpunga ambao unalimwa sehemu za Tunduru na Songea vijijini, korosho ambazo zinalimwa sehemu za Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Mbinga na Songea vijijini na tumbaku maeneo yaNamtumbo,Mbinga na Songea vijijini.
Alisema, Ruvuma imekua ikizalisha chakula kwa kiwango cha utoshelezi na ziada kwa kipindi cha mwaka 2012 - 2013, 2013 - 2014 hali hiyo imeendelea kuwa nzuri hadi kipindi cha mwaka 2015 - 2016. Mahitaji yakiwa ni tani 469,172 na ziada ikiwa tani 1,950,111, ametaja baadhi ya sababu za ongezeko hilo la tani ni pamoja na matumizi ya dhana bora za kilimo, matumizi ya pembejeo za kisasa na urahisi wa upatikanaji wa pembejeo, aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye jana (Jumapili, Januari 3, 2016) ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma, leo siku ya jumatatu atakuwa na shughuli za kufungua tawi la Benki ya Posta mjini Songea, kukagua maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) kanda ya Songea na kukagua Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Kupitia ziara hii Serikali ina lengo la kuona hali halisi ya utendaji wa shughuli za maendeleo kutoka kwa watendaji mbalimbali, kuwatia moyo na kuweka msisitizo katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika sekta ya Afya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,11410 -DAR ES SALAAM
JUMATATU, JANUARI 4, 2016.