Machangu: Magufuli ametunyoosha
Richard Bukos na Issa Mnally
NJAA KALI! Wadada wanaojihusisha na biashara ya kuuza miili yao maarufu kama machangudoa, wameibuka na kupaza sauti kuwa kasi ya Rais John Magufuli ikiwa ni pamoja na kukomesha ufisadi kwa staili ya kutumbua majipu, imewanyoosha kwani wateja sasa wameanza kuadimika.
Wakizungumza jijini Dar kwa nyakati tofauti, akina dada hao walisema wateja wao wakubwa walikuwa ni watumishi wa serikali, lakini hivi sasa wameadimika, kwa wengine kufukuzwa kazi au kubanwa kwa mianya iliyowapatia fedha nyingi isivyo halali.
….Wakiikimbia kamera.
“Kimsingi ni kwamba Rais Magufuli ametunyoosha, wateja wamepungua sana na hata wachache wanaopatikana, kiasi cha fedha wanachotupatia ni tofauti kabisa, inawezekana kabisa wengi wao ni waathirika wa tumbua majipu inayoendelea, kama hakutakuwa na mabadiliko, itabidi kuangalia namna nyingine ya kuishi,” alisema Feb Nayi anayepatikana Sinza Afrika Sana.
Katika viunga vya Mwananyamala, mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Aisha, alisema oparesheni tumbua majipu inawaathiri watu wengi, tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiria.
“Mtu akisikia fulani katumbuliwa jipu, anafikiri labda wanaoathirika ni yeye na familia yake tu, hapana, kuna msururu mrefu wa watu wanaojikuta majipu yamewatumbukia, watu kama sisi tuliokuwa tukiwatoa uchovu kabla hawajafika majumbani kwao, sasa tunalia njaa, kuna wenye migahawa, grosari na hata waosha magari.
“Watu wanatumia kwa uangalifu sana, kwanza hawana uhakika na kesho yao. Zamani nilipata elfu ishirini kwa tendo moja la haraka, lakini sasa hivi hali imekuwa ngumu hadi elfu tano hauiachi,” alisema Aisha anayefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Kilio cha kukosekana kwa wateja wa maana kilikuwa pia kwa machangudoa wa maeneo mengine waliohojiwa kama Buguruni, Manzese, Kariakoo, Kigamboni, katikati ya jiji na maeneo ya pembezoni yaliyo maarufu kwa biashara hiyo.