TRA wampa presha Masanja



Mwimba nyimbo za Injili na mchungaji, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji.

MUSA MATEJA
2016, kazi imepamba moto! Zoezi linaloendelea kufanywa na maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) la kuhakikisha kila mtu analipa kodi inavyotakiwa ili kuipa hazina mapato, sasa limetua kwa mchekeshaji, mwimba nyimbo za Injili na mchungaji, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji,’ tembea na Ijumaa Wikienda.

Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, mfanyakazi mmoja wa TRA Tawi la Kinondoni, Dar (jina lipo) alisema mamlaka hiyo imebaini kuwa, mastaa wengi Bongo na watu wa kawaida, wamekuwa wakinunua magari kimagumashi (kukwepa kodi), hivyo wameamua kuanza kuwasaka watu hao.

Mjengo anaomiliki Masanja.

TWENDE NA CHANZO
“Mtu kama Masanja, tuna taarifa ana magari kama sita, tena mengine ya bei mbaya. Lakini ukimtafuta kwenye system (mfumo) hakuna jina lake. Sasa sijui anatumia jina gani kulipia kodi ya magari hayo.”

KUNA NINI KWANI?
Chanzo hicho kiliendelea kuweka wazi kuwa, hivi karibuni katika uchunguzi wao, TRA walibaini kuwa, msanii huyo amenunua gari la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser Super Charger lenye thamani inayokadiriwa kufikia shilingi milioni mia mbili (200,000,000).

ANATANUA NALO MITAANI
“Masanja anatanua na gari hilo mitaani bila wasiwasi. Sisi tulimwangalia kwenye system hatumuoni.

Kuna wakati tuliamini huenda analipia kodi kwa jina la Masanja maana sisi tunajua anaitwa Emmanuel,” alisema mfanyakazi huyo.

MASANJA ANASAKWA
Mtumishi huyo akaongeza: “Tumeshaenda nyumbani kwake, Tabata Aroma karibu mara tatu lakini hatujamkuta. Tunakuta ndugu zake tu. Lengo letu ni kuona document (nyaraka) ili tujue uhalali wake katika umiliki wa magari hayo.”

MASTAA, WATU WA KAWAIDA WAMO
“Lakini zoezi hili la kukamata magari ya wamiliki waliokwepa kodi si kwa Masanja tu, mastaa wote wamo lakini pia na watu wa kawaida.

Hapa lengo si majina bali ni serikali ya Magufuli inataka mapato. Si unajua malengo ya serikali ya awamu ya tano ni mengi, bila mapato hayatatimia na Magufuli si unajua anavyotumbua majipu, hatutaki kutumbuliwa sisi.”

MASANJA AONGEA NA WIKIENDA
Ili kuweka sawa mzani wa habari hii, Ijumaa Wikienda lilimsaka kwa njia ya simu, Mchungaji Masanja na kumuuliza kuhusu madai hayo ambapo alisema:

“Kwanza mimi sina taarifa za kutafutwa. Kama ni watu kuja kuniulizia nyumbani kwangu ni wengi sana kwa siku. Ikitokea wakaja, nitamalizana nao juu kwa juu maana sioni kama kuna sehemu nimekwenda kinyume na utaratibu wa serikali kuhusu mapato yao. Halafu mimi sina utajiri wa kiasi hicho.”

….Akiwa na moja ya mkebe anaomiliki.

WEMA ALISHAKUMBANA NAO
Mwezi mmoja uliopita, staa wa sinema za Bongo, Wema Sepetu alidaiwa kukumbana na rungu la TRA kuhusu ushuru wa gari aina ya Range Rover Evogue ambalo alilinadi kwenye sherehe yake za kuzaliwa kwamba alilinunua jipya kwa shilingi milioni mia mbili.

Wema alikiri kuzukiwa na watu hao huku akisema msaidizi wake (hakumtaja jina) ndiyo alimalizana na watu hao wa TRA.

WOLPER ALISIKIA
Mbali na Wema, mcheza filamu mwingine wa Bongo, Jacqueline Wolper naye aliwahi kuzungumza na gazeti hili na kusema amesikia watu wa TRA wameanza kuwasaka mastaa wa Bongo kuhusu ushuru wa magari wanayomiliki.

Alhamisi iliyopita, gazeti hili lilitinga kwenye ofisi za TRA Tawi la Kinondoni maeneo ya Mwenge, Dar ili kupata mzani wa habari hiyo lakini hakufanikiwa kumpata msemaji kufuatia kila ofisa aliyefikiwa kudai siyo msemaji wa mamlaka hiyo.


ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …