LOWASSA Akerwa Wafuasi wake Kupigwa Mabomu!

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa ameeleza kusikitishwa na kitendo cha polisi kuwapiga mabomu wananchi wa Tanga waliokuwa wakitoka kwenye mkutano wake.

Lowassa alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Korogwe baada ya juzi kulazimika kuvunja mkutano wake kutokana na wingi wa watu na kusababisha wananchi wengi kuzimia mjini Tanga.

Baada ya kuvunja mkutano huo, polisi walipiga watu mabomu ili kuwatawanya jambo ambalo Lowassa alisema limemsikitisha na kuwaomba waache kufanya hivyo na badala yake watoe ushirikiano kwa wananchi.
“Nasikitika polisi kupiga mabomu. Tushirikiane katika jambo hili ili kuondoa vurugu,” alisema Lowassa huku akiwashukuru wananchi wa Tanga kwa mapokezi makubwa aliyoyapata.

Lowassa, ambaye jana alifanya mikutano ya aina yake akielekea Dar es Salaam kwa gari, alisimamishwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wametanda barabarani katika Jimbo la Muheza na kuhutubia akiwa juu ya gari akisema anahitaji kura za kutosha ili aweze kuleta mabadiliko ambayo wananchi wanayahitaji.

Wananchi hao wa Muheza walimtaka Lowassa awaeleze atafika lini kufanya mkutano mkubwa hapo na atawasaidiaje kutatua tatizo la kutozwa ushuru kwa vitu vidogovidogo.

Lowassa aliahidi kulishughulikia tatizo hilo la ushuru kwa kuliwekea utaratibu maalumu atakapoingia Ikulu na kwamba kabla ya kampeni kuisha, atafika Muheza kuzungumza na wananchi hao.

Akiwa njiani kwenda Korogwe, Lowassa alikutana na umati mkubwa wa watu barabarani ambao walikuwa wakielekea Korogwe mjini ambako alihutubia na kuwaeleza kwa nini ameamua kugombea urais.
Aliwaambia wakazi hao kuwa umaskini umekithiri na mambo kuwa hovyo, hivyo ameamua kugombea ili kuyashughulikia na atawasaidia katika elimu, afya na kilimo.
“Hapa mkoani kwenu nitafufua Bandari ya Tanga ambayo ndiyo itainua uchumi wa mkoa huu,” alisema Lowassa.

Akitokea Korogwe kuelekea Dar es Salaam, umati mkubwa wa wananchi ulisimamisha msafara wake katika eneo la Michungwani jambo lilimfanya asimame tena na kuhutubia kwa dakika saba akiwaomba wamchague ili aboreshe sekta ya elimu na kuifufua Bandari ya Tanga.

Msafara mgombea huyo ulipofika Kabuku ulisimamishwa tena na polisi walifanya kazi kubwa kuwaweka wananchi pembeni huku magari yakikaa kwenye foleni na kusubiri Lowassa ahutubie.
Wananchi hao walisema kuwa kuanzia asubuhi walikuwa wanasubiri ‘mabadiliko’.

Lowassa aliwaomba kura wananchi hao kwa kuwahoji, “mtanipa kura zenu?” nao wakajibu; “tutakupaaaaaaa”.
Lowassa alisema atawatatulia tatizo la maji ambalo linawakumba wakazi wa Kabuku kwa muda mrefu.

Wananchi hao walimwonyesha maji wanayokunywa jinsi yalivyo machafu na baada ya kuyaona alisema wakimpa kura, atahakikisha wanapata majisafi na salama.

Akiendelea na safari, alikuta umati mwingine wa wananchi alipofika Komkonga ambako aliwaahidi kushughulikia tatizo la maji na hospitali, mambo ambayo wananchi wa hapo walimweleza kuwa ni kubwa kwao.

Alitumia dakika tatu kuwaomba kura ili akiwa rais, awatatulie matatizo yao. Baadaye alisimama na kuhutubia eneo la Mkata.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini