Makanisa mengine matatu yavunjwa na kuchomwa moto




Mfululizo wa uhalifu dhidi ya makanisa mbalimbali bado unaendelea katika Mkoa wa Kagera ambapo makanisa matatu yamevunjwa na samani zake kuchomwa moto ndani ya siku moja likiwa ni tukio la pili kutokea katika kipindi cha wiki mbili sasa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Augustino Ollomi amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kwamba jeshi la Polisi bado linaendelea na upelelezi kuhakikisha linawatia mbaroni wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.


Makanisa yaliyoguswa na uhalifu huo ni pamoja na Kanisa la Kilutheri la Katoro na lile la kijiji cha Musira ,pamoja na kigango cha Katoliki cha kijiji cha Kituntu katika tarafa ya Katoro.
Uhalifu huo umefanyika kwa staili ya kuvunja milango na kuchoma samani za ndani ,tofauti na uhalifu wa wiki iliyopita ambapo makanisa matatu ya kipentekoste yalichomwa moto na kuteketea samani pamoja na majengo.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera SACP Augustino Ollomi licha ya kuthibitisha kutokea kwa uhalifu huo,anaelezea mikakati inayowekwa na jeshi hilo kuhakikisha uhalifu huo hautokei tena katika nyumba za ibada.


Aidha Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo John Mongella,ametoa tamko mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa juu ya matukio hayo.


Hii ni mara ya pili ndani ya kipindi cha wiki mbili uhalifu kutokea katika makanisa ,ambapo September 22 makanisa matatu ya kipentekoste katika manispaa ya Bukoba yaliteketezwa kwa moto huku watuhumiwa saba wakishikiliwa kwa ajili ya upelelezi zaidi.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini