Tume ya taifa ya uchaguzi yashangaa madai ya Mbowe


MKURUGENZI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima amedai kushangazwa na taarifa za kuondolewa kwa baadhi ya watumishi wa tume hiyo na kuingizwa wapya wanaotajwa kuwa Usalama wa Taifa (TISS).

Amesema, vyombo vya usalama vimeimarisha ulinzi kwenye Ofisi za NEC lakini hakuna ukweli wa taarifa kwamba, Usalama wa Taifa ‘wameajiriwa kwa kazi maalumu’ kama inavyoelezwa.

“Ni kweli ofisi zetu za tume zinalindwa zaidi kwa sasa na vyombo vya usalama kuanzia Makao Makuu yetu mpaka wilayani ili vifaa vya uchaguzi viwe salama na sio vinginevyo kama inavyopotoshwa kuwa Maofisa Usalama wa Taifa wamejaa,” anasema.

Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Freeman Mbowe wakati akihutubia mkutano wa hadhara juzi kwenye Jimbo la Vunjo, Kilimanjaro alisema,“NEC haipo salama tena kwani imeingiliwa na watu wa Usalama wa Taifa kwa sasa.”

“viongozi wengi wa Tume ya Taifa Uchaguzi kwa sasa wanaondolewa na nafasi zao kuchukuliwa na watu wa Usalama wa Taifa ili kuweza kufanikisha malengo ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kushinda kwa hujuma katika uchaguzi huu,” Mbowe amenukuliwa.

Akizungumza moja kwa moja kupitia Kituo cha Redio cha Magic FM jana asubuhi, mkurugenzi huyo alisema, kauli zinazotolewa na Mbowe si za kweli.

“Sheria za nchi huwa hazisimami kupisha uchaguzi mkuu, rais anayo mamlaka ya kisheria ya kuteua kiongozi yoyote kwa mujibu wa mamlaka yake na sheria za utumishi wa Umma zinaruhusu mtu kuhamishwa eneo la kazi. Shida iko wapi?” alihoji Kailima.

Kuhusu uteuzi huo kufanywa kwa lengo la kisiasa na kutengeneza mazingira ya ushindi kwa CCM, Kailima alikana kuwepo kwa uhalisia wa taarifa hizo.

“Wanaofuatilia masuala ya kisiasa watakubaliana na mimi hata mwaka 2000, 2005 na 2010 watumishi wa tume walikuwa wakibadilishwa karibu na kipindi cha uchaguzi, sasa sijui huu uzushi unaosemwa una lengo gani?” Alihoji.

Hofu imetanda miongoni mwa vyama vya upinzani kutokana na panga pangua ya watumishi wa NEC inayofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika kipindi hiki cha karibia uchaguzi.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini