ALIPUKIWA NA BOMU AKISHAMBULIA POLISI
Askari WP 8616 Mariam, akiwa amelazwa
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ruvuma jana, baada ya kujeruhiwa na
bomu la kienyeji la kurushwa kwa mkono lililotaka kurushwa kwa askari
hao waliokuwa doria wakati wa sherehe za Krismasi eneo la Kotazi, mjini
Songea juzi na kumuua mtu mmoja anayedaiwa kutaka kufanya shambulio
hilo. Picha na Joyce Joliga
Songea. Mtu mmoja mwanaume ambaye jina
lake halikufahamika mara moja, amefariki dunia baada ya kulipukiwa na
bomu wakati akijaribu kuwarushia polisi waliokuwa doria wakati wa
Sikukuu ya Krismasi katika Kata ya Majengo, mjini hapa.
Baada ya bomu hilo kulipuka, lilimpasua
tumbo mtu huyo na kumkata mkono wa kushoto ambao haukuonekana eneo la
tukio. Pia liliwajeruhiwa polisi wawili.
Polisi mkoani Ruvuma ikishirikiana na
makachero kutoka makao makuu ya jeshi hilo, imesema linawasaka watu
wengine watatu ambao wanasadikiwa kujihusisha na ulipuaji mabomu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye
ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Naibu Kamishna wa
Jeshi la Polisi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jina nchini
(DCP), Diwani Athumani alisema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 1.30
usiku katika Mtaa wa Kotazi uliopo kata ya Majengo Manispaa ya Songea.
Alieleza kuwa wakati polisi wakiwa katika
doria kulitokea mlipuko wa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu,
lililotengenezwa kienyeji na kuwajeruhi askari wa wawili.
DCP Athumani aliwataja polisi
waliojeruhiwa PC Mselem mwenye namba G 7903 ambaye alijeruhiwa mkono
wake wa kushoto na alitibiwa na kuruhusiwa na mwingine PC Mariam mwenye
namba WP. 8616 alijeruhiwa kwenye bega la mkono wa kushoto na amelazwa
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ruvuma (HOMSO) akiendelea kupata
matibabu.
DCP Athumani alieleza kuwa wahalifu hao
watakamatwa kirahisi kwa kuwa baada ya mwenzao kulipukiwa na bomu hilo
walijaribu kutorosha mwili wake ili kupoteza ushahidi, lakini
walishindwa baada ya polisi wengine kufika eneo la tukio hilo mapema.
"Wahalifu hao waliuvuta mwili wa mwenzao
kutoka katika eneo la tukio kwa umbali wa mita zisizopungua 80 na 90 kwa
lengo la kutaka kupoteza ushahidi, lakini waliwahiwa na polisi wengine
wa doria na kuuacha mwili na kutokomea kusikojulikana," alisema DCP
Athumani.
Alisema kuwa kikosi chache kimejipanga
kukabiliana na ongezeko la matukio ya mabomu nchini na hususan mkoani
humo, ambapo hilo ni tukio la tatu kwa mwaka huu.
Hata hivyo, amewaomba wadau mbalimbali
wakiwamo viongozi wa dini, wanasiasa, wazee, makundi mbalimbali ya
kijamii pamoja na waandishi wa habari kuwa kitu kimoja katika
kuwafichuwa waharifu hao ili matukio hayo yasiweze kujirudia tena
hususan Mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,
Said Mwambungu aliyetembelea eneo la tukio alisema kuwa waharifu hao
wanaishi kwenye jamii hivyo ni vyema kuwafichua ili mkoa uendelee kuwa
na amani.
"Nimeumizwa sana na vitendo hivi vya
ulipuaji mabomu, naomba wananchi tuwafichue watu wanaofanya vitendo hivi
kwani tunaishi nao kwenye jamii tuache kuyafumbia macho matendo haya
mabaya ambayo ni hatari kwa jamii," alisema Mwambungu.Naye Mganga Mkuu
Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedkto Ngaiza amethibitisha
kupokea mwili mmoja wa mtu ambaye amekufa na utumbo ukiwa umetoka nje.
Pia majeruhi wawili ambao ni polisi na kwamba mmoja alitibiwa jana na
kuruhusiwa huku mmoja akiwa amelazwa wodi ya majeruhi namba mbili
akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri
.CHANZO:MWANANCHI