MWANAHARAKATI AVAA GUNIA NA KUTINGA OFISI ZA JIJI KUMDAI MKURUGENZI WA JIJI LA MWANZA AMLIPE FEDHA ZAKE
Mwanaharakati John Masweta akiwa kwenye geti kuu la Makao Makuu ya Jiji la Mwanza.…
Barua ya shukrani kwa Kampuni ya Tanzania Environment & Conservation (TECO) inayomilikiwa na Masweta.
Na Johnson James, Mwanza
MKURUGENZI
wa Jiji la Mwanza, Halifa Hassan Hida ameingia katika kashfa nzito
baada ya mwanaharakati aliyefahamika kwa jina la John Masweta kutinga
kwenye geti kuu la Makao Makuu ya Jiji la Mwanza jana huku akiwa amevaa
gunia kumshinikiza mkurugenzi huyo amlipe shilingi 1,600,000 aliyopewa
kama zawadi na uongozi wa mkoa na mkurugenzi huyo kushindwa kuilipa
fedha hiyo kwa wakati.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Mwanza kwenye lango kuu la kuingia ofisi
za jiji hilo, Masweta alisema kuwa yeye ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa
Kampuni ya Tanzania Environment & Conservation (TECO) aliyejitolea
kwa zaidi ya miaka 20 kupanda miti na amekuwa akipewa tuzo mbalimbali
kutokana na kazi hiyo na kuweza kuliokoa taifa katika majanga ya jangwa.
Masweta
ameendelea kufafanua kuwa katika kuhakikisha analisaidia taifa, amepanda
miti katika maeneo mbalimbali jijini Mwanza na wakati akiendelea
kupanda miti hiyo akawa amepatiwa tuzo ya mwanaharakati bora kwa kutunza
mazingira iliyoambatana na fedha taslimu shilingi milioni moja na laki
sita lakini cha kushangaza mkurugenzi amekataa kutoa fedha hiyo na
badala yake amempatia cheti tu bila kumpatia na fedha.
Katika
hatua nyingine, Masweta ameendelea kusema kuwa yeye hakupanda miti kwa
lengo la kulipwa na taifa bali alipanda miti ili kuliondoa taifa katika
janga la kukumbwa na jangwa lakini cha kushangaza kila anapotiwa moyo
kwa kupatiwa fedha kidogo, fedha hiyo huishia mikononi mwa watu wengine
ambao hawana huruma na maisha yake.
Hata
hivyo, Masweta alikuwa na mabango yaliyoandikwa ujumbe mbalimbali kama
Toa nguvu zako kwa kulitumikia taifa, uwe faida kwa jamii na taifa, onea
huruma tumbo lako kula mpaka sisimizi, Udhalimu wa Mkurugenzi wa Jiji
la Mwanza haukubaliki.
Masweta amesema kuwa hatoki kwenye lango hilo hadi pale mkurugenzi huyo atakapompatia kiasi hicho cha fedha anazodai.
Aidha
Masweta ametoa rai kwa raia kwa kusema kuwa yeye ni mgonjwa wa kisukari
na hajanywa maji yoyote tokea asubuhi endapo akifariki basi wafahamu
kwamba aliyesababisha kifo chake ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza
kutokana na kuwa na nia ya kudhulumu haki za wenzake.
CREDIT:GPL