Maandalizi ya kujifungua salama kwa mama Mjamzito…




Shirika la Afya Ulimwenguni linasema; kila siku karibia wanawake 800 hufa kwa matatizo ya mimba na uzazi yanayoweza kuzuilika. Asilimia 99 ya vifo vya kina mama wajawazito hutokea kwenye nchi zinazoendelea. Nusu ya vifo hivi hutokea nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, ikiwemo na Tanzania.
Hatari ya vifo vya kina mama wajawazito ni kubwa zaidi kwa mabinti walio na umri chini ya miaka 15 na matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua ndio chanzo kikubwa cha vifo hivyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, mwaka 2013 wanawake 289,000 walikufa kwa matatizo ya mimba na uzazi. Uwiano wa vifo vya kinamama wajawazito katika nchi zinazoendelea kwa mwaka 2013 ni vifo 230 kwa kila vizazi hai 100,000 wakati ni vifo 16 tu kwa kila vizazi hai 100,000 kwa nchi zilizoendelea.
Kadiri mwanamke anavyofahamu mambo mengi zaidi kuhusu mimba yake ndivyo alivyo na nafasi nzuri ya kufanikiwa kujifungua kwa usalama. Kwa kujitunza kabla na wakati wa kujifungua na kufikiria kimbele mambo mbalimbali yanayohusiana na kujifungua, mwanamke atakuwa amefanya yote awezayo kuhakikisha mimba yake ni salama.
Matatizo makubwa ya wakati wa ujauzito na kujifungua yanayobeba karibu asilimia 75 ya vifo vyote vya kina mama wajawazito ni kupanda kwa shinikizo la damu wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua(Kifafa cha mimba).
Uchunguzi unaonyesha kwamba mwanamke anapokuwa mjamzito, magonjwa ya fizi yanaweza kusababisha kifafa, tatizo baya sana ambalo dalili zake zinatia ndani kupanda ghafla kwa shinikizo la damu, maumivu makali ya kichwa na kuvimba kwa mwili kwa sababu ya kuongezeka kwa maji. Kifafa cha mimba kinaweza kumfanya mjamzito ajifungue kabla ya wakati unaofaa mara nyingi watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wao viungo vyao havitokezi chembe nyekundu za damu na kufanya watoto hao kupungukiwa sana damu na kufa haraka na ndicho kisababishi kikuu cha vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua hasa katika nchi zinazoendelea.
Matatizo makubwa mengine ni pamoja na kutokwa damu sana(hasa baada ya kujifungua), maambukizi/magonjwa(hasa baada ya kujifungua), matatizo wakati wa kujifungua mfano mtoto kukaa vibaya tumboni na utoaji wa mimba usio salama.
"Kipimo kilichofanywa kinaonyesha umenasa ujauzito". Ni maneno kutoka kwa mhudumu wa afya yanayoweza kupokelewa na mwanamke kwa furaha au huzuni. Hii hutokana na utayari wa mwanamke kuwa mama au la. Makala haya yatalenga upande wa wanawake wanaopokea habari ya ujauzito kwa furaha na walio tayari kulea mimba hadi kujifungua. Akina mama wengi hutazamia kujifungua watoto wenye afya na walionenepa, lakini hawatendi mambo kama wanavyotarajia.
Baadhi ya mambo yanayosababisha matatizo wakati wa Kujifungua: 
  • Kutojitunza vizuri kwa manamke kipindi cha ujauzito. Afya ya mama na mtoto aliyezaliwa vina uhusiano wa karibu sana. Akina mama wenye afya nzuri hujifungua watoto wenye afya nzuri.
  • Kukosa matibabu yanayojulikana sana, yanayofaa na yasiyohitaji vifaa tata. Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinadai watoto waliozaliwa karibu ya milioni 3 hufa kila mwaka na watoto milioni 2.6 huzaliwa wakiwa wamekufa. Jarida la UN Chronicle linaripoti kwamba asilimia 66 ya watoto wanaokufa wanapozaliwa wangeweza kuzuiwa ikiwa akina mama na watoto hao wangepata matibabu yanayojulikana sana, yanayofaa na yasiyohitaji vifaa tata.
  • Kukosa huduma nzuri za afya kipindi cha ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua. Jarida la UN Chronicle linasema kwamba mwamamke asipopata huduma nzuri za afya anapokuwa mjamzito, anapojifungua na baada ya kujifungua, mtoto wake pia hatapata huduma za afya.
  • Je, kupata huduma nzuri za afya kunamaanisha kwenda kliniki kila juma? La, si lazima. Kuhusu matatizo ya kawaida yanayowapata wanawake wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua, Shirika la Afya Ulimwenguni liligundua kwamba wanawake walioenda kliniki mara nne tu wakati wa ujauzito walipata matokeo yale yale kama wanawake walioenda kliniki mara 12 au zaidi.
  • Kukosa usafiri tokana na umbali wa huduma za afya. Idadi kubwa ya raia wa watanzania inapatikana maeneo ya vijijini ambako huduma za afya hazipo za kutosha hivyo kulazimisha wajawazito kusafiri umbali mrefu kusaka huduma bora za afya. Usafiri ni wa taabu na wa gharama sana kitu kinachopelekea wajawazito kushindwa kumudu.Asilimia 47 tu ya wajawazito hujifungua kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, asilimia 46 wanaozaa huhudumiwa na kusaidiwa na wataalamu wa huduma za afya. Kati ya asilimia 53 ya wanaozalia nyumbani, asilimia 31 husaidiwa na ndugu zao, asilimia 19 husaidiwa na wakunga wa jadi na asilimia 3 hujifungua bila msaada wowote.
  • Kutokuwa na uwezo wa kugharamia huduma za afya. Shirika la Afya Ulimwenguni lasema; vifo vya kina mama wajawazito maeneo ya vijijini vipo juu sana hasa kwenye jamii masikini. Wanawake wenye vipato vya juu wanatarajia kujifungua kwa msaada wa wataalamu wa afya kwa asilimia 87 ikilinganishwa na wanawake wenye vipato duni ambayo ni asilimia 13 tu.
  • Kutokuwa na elimu. Wajawazito wengi wanaopata matatizo ni wale ambao hawakusoma au wale hawana taarifa kuhusu afya ya uzazi pamoja na uzazi salama.
  • Mila potofu. Jamii nyingi za vijijini bado wana mila potofu zinazotia ndani kujifungulia nyumbani ambapo huamini anayejifungulia nyumbani ndio shujaa kitu ambacho kinaweza sababisha matatizo kwa kuwa hatopata husuma stahiki.
Umuhimu wa wahudumu wa afya kwenye Uzazi Salama:
Wao huchunguza rekodi za matibabu za mama na kufanya uchunguzi ili kuona kama kunaweza kuwa na hatari na hivyo kuzuia matatizo yanayoweza kumpata mama na mtoto wake. Wakati hatari zaidi kwa mjamzito ni pindi anapopatwa na maumivu ya kuzaa hadi anapojifungua. Wanapotambua hatari zinazohusiana na mjamzito huchukua hatua zinazofaa au kumsaidia mjamzito kuchukua hatua hizo, wanachangia afya nzuri kwa mama na mtoto wake ambaye bado hajazaliwa.
Wanaweza kupima damu na mkojo ili kuchunguza mambo kama vile upungufu wa damu, maambukizo, ikiwa damu ya mama na mtoto hazipatani na magonjwa. Magonjwa hayo yanaweza kutia ndani kisukari, surua ya rubella, magonjwa ya zinaa na ugonjwa wa figo, ambayo yanaweza kufanya shinikizo la damu lipande.
Pia wanaweza kupendekeza atumie vitamini mbalimbali, hasa aina fulani ya vitamini B inayoitwa folic acid na madini ya chuma. Faida za asidi ya foliki ni pamoja na kutengeneza damu, kumkinga mtoto dhidi ya ugonjwa wa mgongo wazi na kuhakiki mfumo wa fahamu. Faida za madini ya chuma ni pamoja na kuimarisha kinga ya mwili, kutengeneza chembechembe nyekundu za damu, kuimarisha uwezo wa kuwa makini na kuongeza uwezo wa kufanya kazi vizuri.
Matayarisho kwa ajili ya kujifungua salama:
  • Baba na mama mtarajiwa afanye utafiti mapema ili na wachague kituo cha afya chenye wahudumu wazoefu na wakutosha. 
  • Mama na baba watarajiwa wamtembelee daktari au mkunga wako kwa ukawaida ili usitawishe urafiki na kuaminiana.
  • Mama atunze afya yake tokana na ushauri wa daktari wake, kwa kula vizuri, kunywa dawa za vitamini zilizoshauriwa na daktari na kupima vipimo vyote muhimu vya afya. 
  • Ikiwa mama mtarajiwa anapata maumivu yoyote makali kabla ya kuzaa awasiliane na daktari wake mara moja. 
Vitu vya muhimu ambavyo mama mjamzito anapaswa kutayarisha kabla ya kujifungua: 
Mama mjamzito ni muhimu akaanza kujiandaa kabla tu ya ujauzito kutimiza miezi saba. Vitu vya msingi ni vitambaa vingi/khanga safi walau doti tatu, pamba kubwa walau miligramu 500, wembe mpya (usifunguliwe mpaka unapohitajika kukata kitovu) kama huna wembe tumia mkasi safi usio na kutu(uchemshe kabla ya kuutumia), sabuni, brashi safi ya mikono na kucham gloves na nguo kwa ajili ya mtoto mara atakapo zaliwa.
Vingine ni vipande vya vitambaa vilivyo safi sana kwa ajili ya kufunika kitovu, spiriti ya kupaka mikono baada ya kuiosha, kamba mbili za nguo za kufungia kitovu au klampi mbili za kubania kitovu, sindano na uzi wa kushonea sehemu iliyochanika ya mbele na dawa ya macho kwa ajili ya mtoto.
Shirika la Afya Ulimwenguni linashauri; 'Ili kuzuia vifo vya kina mama na vichanga, ni muhimu pia kuzuia mimba zisizohitajika na mimba za mapema sana. Wanawake wote ukijumlisha vijana wanapaswa kupata huduma za uzazi wa mpango, huduma za kutoa mimba salama kulingana na sheria pia kupata huduma nzuri baada ya kutoa mimba au  kujifungua.'
Baadhi ya mahitaji hayo huandaliwa hospitali, ila kwa baadhi ya hospitali yenye vifaa visivyotosheleza ni muhimu kujiandaa kwa vitu vyote muhimu.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini