Kigogo Mnyarwanda Chadema akamatwa, kisa si mtanzania
Gaudence Msuya, Mbogwe
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya
Mbogwe mkoani Geita, Omari Athanas, ametiwa mbaroni na maofisa uhamiaji
wilayani hapa, akituhumiwa kwa uhamiaji haramu.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Aman Mwenegoha, alisema mwenyekiti
huyo alikamatwa Desemba 22, mwaka huu na kuhojiwa na maofisa hao, ambapo
alihojiwa kwa muda na kugundulika kwamba, si Mtanzania bali ni raia wa
nchi jirani ya Rwanda.
Alisema taarifa ya kumbaini kuwa, si Mtanzania zilijitokeza wakati wa
kampeni za Serikali za Mitaa, baada ya mwenyekiti huyo wa Chadema
kwenda katika Kijiji cha Lugunga, ambapo inadaiwa kuna Wanyarwanda wengi
na kuwahamasisha wafanye vurugu na kwamba, wasichague CCM kwa kuwa,
Serikali haitaki kuwapa kibali cha uraia.
Kaimu mkuu huyo wa wilaya alisema baada ya mahojiano ya siku tatu,
ndipo maofisa uhamiaji wa wilaya hiyo walipojiridhisha kuwa, si raia wa
Tanzania.
Mwenegoha alisema Desemba 26, mwaka huu waliamua kumsafirisha nchini
Rwanda, ambapo maofisa uhamiaji nchini humo walimtambua kuwa ni
Mnyarwanda, na ana familia yenye mke na watoto wawili.
“Baada ya kumfikisha Rwanda, maofisa uhamiaji walimhoji ambapo
walimtambua kuwa, ni raia wa nchi hiyo na wakati akija Tanzania walimpa
kitambulisho, zaidi ya miaka 15 iliyopita na pia wakamgundua kuwa, ana
familia yenye mke na watoto wawili,” alisema Mwenegoha.
Alifafanua kuwa, alifika nchini toka mwaka 2000 na kuishi katika
Kitongoji cha Manzese Kata ya Busoka wilayani Kahama, na baadaye mwaka
2003 alihamia katika Kijiji cha Lugunga wilayani Mbogwe mkoani Geita,
ambapo aliishi huko hadi alipokamatwa Jumatatu wiki hii.
Kuhusu wahamiaji waliopo katika wilaya hiyo, Mwenegoha alisema ni 14,
ndiyo walioomba kuukana uraia wao na kupewa uraia wa Tanzania na
kwamba, inadaiwa kuwa, ameacha deni la sh. milioni 1.5 ambalo anadaiwa
na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chadema wilayani humo, ambaye alihamia
CCM, ambapo alikopa ili afanikishe kampeni za uchaguzi wa Serikali za
Mitaa.
Aidha, alisema katika tukio hilo imebainika kuwepo uzembe mkubwa
uliofanywa na uhamiaji wilayani humo kwa kushindwa kumbaini mapema
kiongozi huyo, ambapo alisema atakaa na kamati ya ulinzi na usalama wa
wilaya hiyo ili kujadili suala hilo.
Hata hivyo, Mwenegoha alisema kwa sasa wanajipanga kufanya oparesheni
kubwa ya kuwasaka wahamiaji wote haramu ili sheria ichukue mkondo wake,
ikiwemo kuwarudisha kwao watakaobainika.
Kwa upande wake, Ofisa Uhamiaji wilayani hapa, David Magwaza alisema
wamebaini kuwa, mwenyekiti huyo aliingia nchini kijanja na kisha
kujifunza lugha ya kiswahili fasaha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alfonce Mawazo,
alisema hizo ni siasa, huku akihoji kwanini hakukamatwa wakati wote huo
alioishi nchini na badala yake, akamatwe sasa.
Alisema mwenyekiti huyo aliishi nchini kwa muda mrefu, ambapo ana mke na watoto wawili pia.