BINTI ATEKWA NA WACHUNA NGOZI


Binti anayetambulika kwa jina la Latifa Abdallah 
(wa pili kushoto) akiwa na ndugu zake
Stori: Chande Abdallah na Deogratius Mongela
MBONA majanga! Mrembo aliyejitambulisha kwa jina la Latifa Abdallah (19), mkazi wa Kinondoni –Mkwajuni, Dar amesimulia alivyotekwa na watu aliodai ni wachuna ngozi wakiwa na mwanamke aliyevalia kininja ndani ya gari jeusi.


Akizungumza na Uwazi jijini Dar, juzi, Latifa alidai Oktoba 19, mwaka huu akiwa anatoka kumsindikiza dada yake aliyekuwa akienda Kibaha, Pwani ghafla msichana aliyevalia kininja akajigonga kwenye mwamvuli alioushika na kumwambia alimgonga kwa makusudi.
“Nilimwomba msamaha na kumwambia ni bahati mbaya lakini alinikamata na kuniingiza ndani ya gari jeusi lililopaki kando ya barabara ambapo kuna mtu alifungua mlango yule mwanamke akanisukumia ndani,” alisema Latifa.
Akizidi kusimulia, binti huyo alisema kuwa, ndani ya gari hilo alimkuta msichana mmoja kama yeye na mtoto kama wa miaka miwili wakiwa wamefungwa vitambaa vyeusi machoni na yeye akafungwa kama wenzake.
“Tulikwenda kushushwa kwenye nyumba moja sijui ni wapi, tukaingizwa katika  chumba kidogo na kufunguliwa vitambaa. Ndipo nilipogundua kuwa, watekaji wote walivaa kininja. Mmoja alikuwa mwanaume, mwingine ndiyo yule aliyenisukumia ndani ya gari pale kwenye Kituo cha Daladala cha Vijana Kinondoni (Dar).

Fomu ya PF3 ya Latifa Abdalla aliyopewa kituo cha Polisi Oysterbay.
“Yule mwanaume alisema lazima tufanye  naye mapenzi la sivyo atatufanya kama watakavyomfanyia yule mtoto. Wakamchukua yule mtoto na kumchoma sindano, alilia sana kisha akanyamza ghafla huku ngozi yake ikiumuka kama puto. Yule mwanaume alitoa kisu na kuanza kumchuna ngozi yule mtoto akianzia shingoni.
“Nikiwa katika hali ya kutetemeka kwa woga, yule mwanamke alisema tujiandae na kifo kama cha yule mtoto. Nilimwomba Mungu sana atuepushie kifo hicho.
“Siku ya Jumanne asubuhi wale watu walikuja kutuangalia kidogo na kuondoka. Baadaye jioni walirudi na kutupa maji ambayo hatukuelewa ndani yake yalikuwa na nini, walitunywesha na kutuambia kesho yake wangeturudisha makwetu, wakachukua namba za simu za ndugu zetu, sikuamini nikawatajia namba ya mwalimu wangu wa cherehani ambaye waliniambia akipokea nimwambie kuwa mimi ni mzima nitafika nyumbani kesho kutokea Kawe  jambo ambalo nililifanya.
“Kuanzia hapo yule mwanamke akawa anachati naye. Wakati huo yule mwenzangu kwao ni Mbezi naye aliwataarifu ndugu zake na tukawa tunasubiri kesho ifike. Kweli, kesho yake wakatuchukua, mimi nikashushwa pale Kituo cha Daladala Kinondoni–Studio (Dar), wakanipa shilingi 1,000 wakasema nipande bodaboda nirudi nyumbani,” alisema Latifa.
Mwalimu wa cherehani wa Latifa, Celestine ‘Baba Mkanji’ alisema tangu Latifa atoweke nyumbani amekuwa akipigiwa simu na kutumiwa meseji zinazoonesha Latifa alikuwa kwenye hali ya hatari jambo lililomshtua na kuwashirikisha ndugu zake nao wakaripoti Kituo cha Polisi cha Mzambarauni, baadaye Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar.
Baada ya kurudishwa nyumbani, Latifa alipelekwa Oysterbay Polisi kwa ajili ya kupata PF3 na baadaye kwenda Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya vipimo zaidi.
Naye mama mzazi wa Latifa, Habiba Saidi (56) alisema  amesikitishwa na kitendo alichofanyiwa mwanaye na kuomba watu wa haki za binadamu na wanasheria wamsaidie ili waliomfanyia mambo hayo mwanaye wakamatwe.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini