China yamwaga neema kwa Tanzania

SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imetangaza neema
kubwa kwa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kutoa dola za Marekani
milioni 85 (Sh bilioni 140) kwa ajili ya shughuli za maendeleo na
kuisaidia Tanzania kufanya mageuzi ya viwanda.
Neema hiyo ya China kwa Tanzania imetangazwa na Rais Xi
Jinping wa nchi hiyo katika mazungumzo rasmi ya kiserikali kati
yake na ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Rais Jakaya
Kikwete, ambaye yuko katika ziara rasmi ya siku sita nchini
China.
Mazungumzo hayo kwenye Jumba la The Great Hall of the
People, yalifanyika baada ya Rais Kikwete kukaribishwa rasmi
katika Jamhuri ya Watu wa China kwa kupokelewa na Rais Xi
Jinping katika eneo la East Plaza la Jumba hilo.
Katika mapokezi hayo, Rais Kikwete alipigiwa mizinga 21 na
kukagua gwaride la ukakamavu la Jeshi la Ukombozi la
Wananchi wa China.
Katika mazungumzo hayo, Rais Xi Jinping alitangaza kuwa China
itaipatia Tanzania kiasi cha dola za Marekani milioni 85 (Sh
bilioni 140), ikiwa ni mchanganyiko wa msaada na mkopo
usiokuwa na riba, fedha ambazo Tanzania itaamua yenyewe jinsi
gani ya kuzitumia.
“Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania
kuboresha maisha ya wananchi wake, napenda kutangaza kuwa
China itatoa kiasi cha RMB milioni 200 ikiwa ni msaada na RMB
milioni 200 nyingine zikiwa ni mkopo usiokuwa na riba kwa
Tanzania.” “… na kiasi cha RMB milioni 100 za msaada kwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo zitatumika kwa kadri
Serikali hizo mbili zitakavyoamua,” alisema Rais Jinping.
Rais huyo wa China pia alitangaza kuwa nchi hiyo, itaisaidia
Tanzania katika uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji ya EPZ,
uendelezaji wa miundombinu, itaharakisha ujenzi wa Bandari ya
Bagamoyo na itaingia katika shughuli za kutafuta gesi na mafuta
katika ukanda wa Bahari ya Hindi katika eneo la Tanzania.
Rais Jinping pia alitangaza kuwa Serikali ya China imefanya
uamuzi wa kuikarabati Reli ya TAZARA, inayounganisha
Tanzania na Zambia na yenye urefu wa kilomita 1,860 na
kusaidia uendeshaji wa reli hiyo.
“Ili kutekeleza uamuzi huu kwa haraka, napendekeza kuundwa
kwa kamati ya pamoja ya wataalamu kuandaa ramani ya namna
ya kuitoa reli hiyo katika matatizo yake ya sasa,” alisema.
TAZARA ndiyo reli ya kwanza duniani kujengwa na Jamhuri ya
Watu wa China, ambao utaalamu wake sasa unasakwa na nchi
nyingine nyingi duniani.
Rais Jinping pia alitangaza Serikali yake itatoa nafasi 100 za
masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka Tanzania katika
miaka mitano ijayo, itaongeza idadi ya madaktari ambao China
inapeleka Tanzania, itahimiza kampuni zaidi ya China kuwekeza
katika Uchumi wa Tanzania na kuzishawishi taasisi za kifedha
za China kuanzisha shughuli zake katika Tanzania.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini