Tatianala umeme jijini Dar kuendelea hadi Novemba 2, 2014


Tatizo la kukatika kwa umeme litaendelea hadi Jumapili Novemba 2, 2014 ikiwa matengenezo ya mitambo ya uzalishaji umeme ya Tegeta na Ubungo, Dar es Salaam yatakamilika kwa wakati, FikraPevu imefahamishwa.
Tatizo la kukatika kwa umeme limeenza kujitokeza kwa siku kadhaa sasa na taarifa za ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zinaeleza kwamba kuna matengenezo ya kawaida (maintenance) kwa mitambo ya Tegeta na Ubungo.
FikraPevu imebaini kwamba mbali ya matengenezo ya mitambo hiyo, kuna taarifa kwamba wazalishaji wa gesi nao wanafanyia matengenezo ya mfumo wao na kupunguza utoaji wa gesi inayopelekwa kwenye mitambo ya Tanesco kipindi ambacho shirika hilo limemaliza akiba ya nishati hiyo.
Kumekuwa na utata kuhusiana na tatizo la umeme katika baadhi ya maeneo mbalimbali ya nchi likiwamo jiji la Dar es Salaam kutokana na wahudumu wa Tanesco kudaiwa kuudanganya umma wanapopigiwa simu kwamba kuna hitilafu katika eneo husika.
Utafiti wa FikraPevu umebaini kwamba taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwa wateja wa maeneo yote bila kujali utofauti wa kijiografia. Mfano jibu la “Mafundi wetu wanafuatilia, kuna tatizo limetokea hapo mtaani kwenu,” hutolewa kwa wateja wa Ilala, Kariakoo, Temeke, Kinondoni, Kijitonyama,  Tabata, Kimara, Sinza na Upanga.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimeijulisha FikraPevu kwamba kuna wasiwasi wa kuwapo hujuma ama uzembe na wananchi wamehoji “Inakuwaje ‘maintanence’ ya mitambo na mifumo ya uzalishaji umeme ikafanyika kwa wakati mmoja na katika kipindi ambacho akiba ya gesi imekwisha?”.
FikraPevu imejulishwa pia kwamba hivi karibuni Tanesco ilisitisha ununuzi wa umeme kutoka kwa mzalishaji binafsi kutokana shirika hilo kuwa na umeme wa kutosha kutoka katika mitambo yake inayoendeshwa na maji.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini