MWANAMKE ATIWA MBARONI KWA KUIBA MTOTO RUKWA ILI ASIACHIKE KWENYE NDOA YAKE

POLISI mkoani Rukwa wanamshikilia mkazi wa kitongoji cha Chanji,
Manispaa ya Sumbawanga, Magreth Juma (34) akituhumiwa kuiba
mtoto wa kike mwenye umri wa siku mbili ili asiachike katika ndoa
yake, kwa kuwa hajabahatika kumzalia mtoto mumewe.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa,
Jacob Mwaruanda ambaye alisema uchunguzi wa awali umeonesha
mwanamke huyo, kabla ya kuchukua uamuzi wa kuiba mtoto,
alishawahi kuzaa na mwanamume mwingine kabla ya kuwa na
mumewe wa sasa.
Hata hivyo, inadaiwa baada ya kuishi na mumewe wa sasa kwa
zaidi ya miaka miwili bila kupata mtoto mwingine, alihofia kuvunjika
kwa ndoa yake, hasa ikielezwa mumewe alikuwa akidai mtoto.
Mwaruanda alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitiwa nguvuni Oktoba 22,
mwaka huu asubuhi ikiwa ni muda mfupi tangu mtoto huyo aibwe
kutoka kwa mama yake katika kitongoji cha Bangwe.
Aliongeza kuwa awali alfajiri siku hiyo ya tukio, taarifa ziliripotiwa
Kituo cha Polisi Sumbawanga na mama mzazi wa mtoto huyo,
aitwaye Magreth Benias (28) kuwa mtoto wake mchanga amepotea
katika mazingira ya kutatanisha.
“Ndipo polisi kwa kushirikiana na raia wema walianza msako na
muda mfupi baadaye walimkamata mtuhumiwa akiwa na mtoto
huyo nyumbani kwake...tulibaini kuwa mama wa mtoto huyo na
ndugu wa mtuhumiwa waliwahi kuishi nyumba moja ya kupanga
ambapo mtuhumiwa alikuwa akifika katika nyumba hiyo
kumtembelea ndugu yake,” alieleza.
Kamanda Mwaruanda alisema mtoto huyo aliyeibwa, amekabidhiwa
kwa mama yake mzazi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu
wa afya yake.
Alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi
wa awali wa shauri lake kukamilika.
Na Peti Siyame, Sumbawanga

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini