Majambazi yateka mabasi 6 jijini Arusha....Abiria Wavuliwa nguo na kuporwa, Wanawake wanyang'anywa hadi shanga na vitu vingine vya ndani


WATU zaidi ya 40 wanaodhaniwa kuwa majambazi, wameteka mabasi sita ya abiria yanayofanya safari kati ya Jiji la Arusha na Nairobi, Kenya na kupora mali na fedha ambavyo thamani yake haijafahamika.

Tukio hilo ambalo limethibitishwa na Jeshi la polisi, mkoani Arusha llitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Mbuga Nyeupe, wilayani Longido Mkoa wa Arusha baada ya watu hao kuweka mawe barabarani na kuwamuru abiria wote kutemka mmoja baada ya mwingine, kulala chini na kuwapekua kila kitu walichokuwa nacho.

Akisimulia mkasa huo, dereva wa basi la Perfect Trans, Joseph John, alisema kuwa watu hao waliokuwa na silaha za jadi yakiwamo mashoka, mapanga  na sime, waliteka mabasi hayo majira ya saa 8 usiku.

“Hao jamaa walikuwa kama 50  hivi kwani waliteka magari yetu ambayo yalikuwa yamefuatana, wametuvua hadi viatu, saa yaani walipekua hadi wanawake waliamriwa kuvua nguo na kuporwa urembo wenye nakshi ya madini ya vito,” alisema John.

Alisema yeye alikuwa dereva wa kwanza kufika na basi katika eneo hilo na kuwa alipoona mawe yamepangwa kati kati ya barabara, aliamua kusimama  na alipokuwa akijaribu kuyakwepa, alipigwa jiwe usoni hali iliyomfanya ashindwe kukimbia.

“Hata wengine walikuwa hawajafunika nyuso zao, tukio lilidumu kwa dakika zaidi ya shirini, kila walipomaliza kupekua watu wa basi moja waliwaamuru warudi ndani ya gari,” alisimulia.

Dereva mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jabir Athumani, alisema  baadhi ya majambazi hayo yalikuwa yakiita majina ya baadhi ya watu na kuwaamuru kutoa fedha walizokuwa nazo.

“Tunaomba vyombo ulinzi na usalama vifuatilie tukio hili kwa umakini wa hali ya juu ili kuwanasa wahusika wa tukio hili,” alisema Jabir.
 
Aidha, alililitaka Jeshi la Polisi lirudishe magari ya doria  katika barabara ya Arusha–Namanga ambayo yaliondolewa Aprili mwaka jana.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi leo.

“Hapa nipo katika majukumu mengine, sipo ofisini nitawapa taarifa za tukio lote Jumatatu (leo) mchana, naomba subiri nitafanya mkutano na vyombo vya habari na nitawapa maelezo ya tukio lote,” alisema Sabas.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini