Chadema, CCM Wachuana Vikali Matangazo ya Televisheni!

Vyama vya Chadema na CCM vimeingia katika mchuano wa kuwania nafasi ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya kampeni za wagombea urais katika televisheni Jumamosi hii.
Wakati Chadema ikitaka muda wa kurusha matangazo ya uzinduzi wa kampeni za mgombea wake, Edward Lowassa kutokea jijini Dar es Salaam, CCM inataka kurusha matangazo ya mkutano wa kampeni ya mgombea wake, Dk John Magufuli kutoka jijini Mbeya.


Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema jana kuwa kumekuwa na njama za CCM kutaka kuzuia fursa ya Chadema kurusha kampeni za mgombea wake kwa kutaka siku hiyo irushe kampeni za Dk Magufuli.

Akizungumzia madai hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikiri chama hicho kutaka kurusha matangazo ya mgombea wake na kuhoji; “tatizo liko wapi kama Chadema imechelewa kulipia?”

“Ni kweli mgombea wetu wa urais akiwa Mbeya tutarusha matangazo ya kampeni zake moja kwa moja kwenye runinga, sasa ni runinga ngapi siwezi kujua maana kuna watu wanalifanyika kazi suala hilo. Lakini kama Chadema walijua wana tukio lao kwa nini wasingewahi kulipia?” alihoji.

Chanzo cha habari kutoka kituo kimoja maarufu, kimeeleza kuwa kwa nyakati tofauti, CCM na Chadema waliomba muda wa kurusha vipindi vyao, lakini CCM ndiyo waliofanikiwa kupata.
“Ninachojua hao wote walikuja kwa nyakati tofauti kuomba muda na CCM ndiyo waliofanikiwa kupata,” alidokeza mmoja wa wafanyakazi wa telesheni hiyo ambaye hakutaka kutaja jina kwa maelezo kuwa siyo msemaji.


Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV, Tido Mhando alisema CCM na Chadema vilikuwa vimeomba kurushiwa matangazo yao na vyote vimelipia. Alisema kila moja kitapata fursa hiyo kwa kuwa kituo chake kina channel nyingi.

Hata hivyo, mmoja wa wahariri wa Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1), alisema: “Sisi tunarusha vipindi vyetu kulingana na matukio na mahitaji ya jamii, hatuko fixed.” Alieleza kuwa ameamua kutoa jibu hilo rahisi kwa kuwa alijua kwa nini mwandishi aliuliza.

“Sisi hatuna utaratibu wa kurusha live (moja kwa moja), wanaofanya hivyo ni watu wa radio tena huwa hilo linafanywa kibiashara. Kwamba wateja wanaomba kutangaziwa vipindi vyao na kulipa fedha,” kilieleza chanzo kutoka kituo kingine.

Habari zimeeleza kuwa kituo kimoja kikubwa cha televisheni kimethibitisha kurusha matangazo ya mgombea wa Chadema.
Awali, Makene alisema hadi jana, chama hicho kilikuwa kimefanikiwa kupata vituo vinne na radio nne.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …