MOI yafurika majeruhi wa ajali, wengine walazwa sakafuni
Kuongezeka kwa majeruhi wa ajali za bodaboda kumeifanya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), kuzidiwa na wagonjwa hadi kulazimika kuwalaza wengine sakafuni.
Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alisema asilimia 53 ya majeruhi wote wanaopokewa na taasisi hiyo ni wa ajali za pikipiki.
Wajumbe wa Kamati ya Usalama Barabarani, Kanda ya Dar es Salaam jana walitembelea wodi namba 17 na 18 za Jengo la Sewahaji na Wodi namba Mbili ya Jengo la Mwaisela na kujionea idadi kubwa ya majeruhi. Majeruhi wengi waliolazwa Sewahaji ni vijana ambao baadhi yao wamekatika miguu, mikono na wengine wakiwa na majeraha vichwani.
Mvungi alisema kila siku taasisi hiyo inapokea majeruhi kati ya 20 na 26 na kwamba wengi wao ni wa ajali za pikipiki. “Wodi za kulaza majeruhi zimezidiwa tunalazimika wengine kuwalaza chini lakini wote wanapata matibabu,” alisema.
Alisema Wodi Namba Mbili, ambayo ni ya majeruhi wanawake, ina vitanda 33 lakini hadi jana ilikuwa na wagonjwa 54 na kwamba waliozidi wanalala sakafuni.