MAKAVU LIVE: Diamond, Diva kwani ‘vepe’, MMEJISAHAU eeh?!


KUNA baadhi ya nyakati unajikuta unashangazwa na baadhi ya maneno unayoweza kuyasikia kutoka kwa watu unaowaheshimu, hasa yanapotolewa hadharani.
Binadamu tumeumbwa tukiwa na udhaifu mwingi, ingawa wapo baadhi ya wenzetu, licha ya kujua kuwa hakuna asiye na upungufu, wamekuwa hodari wa kuhubiri ya wenzao, huku yao, ambayo ni mabaya zaidi, wakiyaweka kando.

Na lipo pia tatizo la vijana wa mjini, kuelemewa sana na maneno ya mjini, ambayo wakati mwingine, kwao matusi huwa ni sifa, yaani anamtukana mtu, lakini kwa kumsifu na hata mikono wanagongesheana!

Kuna maneno kijana wa mjini anaweza kuyaongea mbele ya vijana wenzake yakawa yanaeleweka na wala asiwepo mtu wa kuyahoji uhalali wake, lakini maneno hayohayo, kwa baadhi ya watu yakawa hayatamkiki na hayavumiliki.

Huu ni umjini ambao hata hivyo, hauondoi ukweli kuwa kilichotamkwa, kwa tamaduni zetu, ni tusi. Kwa maana hiyo, kimsingi mtu anapozungumza kitu kwa lugha ya mjini, ni vyema akatambua eneo alipo, wanaomsikiliza na wakati mwingine hata kuhisi athari zinazoweza kutokea kwa matamshi anayotoa.

Ninamheshimu bwana mdogo Diamond Platnumz kama msanii wa muziki wa kizazi kipya (nachelea kumwita mwanamuziki). Jinsi anavyojituma, anavyotumia fursa anazokutana nazo na hata anavyojithaminisha, ni vitu vya kuvutia na ambavyo vijana wa umri wake wanapaswa kumuona kama mfano, kama maisha yao yanamaanisha kutafuta mafanikio!

Lakini juzikati, alinisikitisha kwa matamshi yake alipokuwa akihojiwa na kipindi kimoja kinachosikilizwa zaidi na vijana kupitia kituo kimoja cha redio maarufu hapa mjini.

Katika kipindi hicho, Diamond alikuwa akifanyiwa mahojiano lakini baadaye, akasikika mtangazaji wa kike Loveness Malinzi ‘Diva’ akiwa pamoja nao. Inavyoonekana, wawili hao (Diamond na Diva) wana ‘kaugomvi’ kao binafsi, kwani kidogo hali ya hewa ilibadilika hadi kuwafanya watoe maneno ambayo hayawezi kuandikwa hapa (matusi).

Kwamba ni hatua gani zitachukuliwa, kwanza na wao wenyewe au na mamlaka zinazohusika, siyo suala ninalotaka kulijadili hapa, bali ninachotaka kufanya ni kuwakumbusha tu wote wawili Diamond na Diva, kuwa wao wana jukumu kubwa sana katika ulimwengu huu wa sasa.

Wote ni vijana na kila mmoja ana jukumu kwa jamii inayomzunguka. Inategemewa Diamond awe wa kwanza kuheshimu maadili yetu kama taifa kwa sababu ‘swaga’ zake zinafuatiliwa na watu wengi, wakiwemo watoto. Vivyo hivyo kwa Diva, kwani kuwa mtangazaji wa redio maarufu ni mzigo.

Naamini wote wanaelewa jukumu lao na hasa wanapokuwa mbele ya kipaza sauti kinachorushwa katika eneo kubwa la nchi. Nilisema pale awali, maneno ya kimjini yana sehemu yake, yana watu wake na zaidi yana muda wake.

Kuleta maneno ya kimjini yenye maana ya matusi katika sehemu nyeti, kwa sababu tu wewe ni msanii mkubwa au mtangazaji mahiri haikubaliki. Ukubwa na umaarufu wa kila mmoja wetu una mipaka inayopaswa kuheshimiwa.

Kutukana kwa namna yoyote hadharani ni kosa kisheria.
Kama kila mtangazaji maarufu atatumia kipaza sauti chake kumtusi mtu mwingine, basi nadhani marafiki zangu kama Paul James, Alex Luambano au Gardner G Habash, wangeshawatusi wengi, maana huku kwenye vikao vyetu vya baada ya kazi kuna maudhi mengi sana.

Na endapo kuwa msanii mwenye jina kubwa ndiyo iwe tiketi ya kuwatusi waandishi, nadhani Diamond angeshawakuta kaka zake kama Dudubaya, Profesa Jay, Fid Q, Mchizi Mox, Jaffarai, TID, Nature na wengine wa kitambo hicho wameshafanya hivyo, maana yameandikwa mengi sana wasiyoyapenda!
Rai yangu kwa watu wote wenye majukumu, hasa ya kuwa mifano kwa jamii, kujihadhari na maneno wanayotamka, hasa yenye mrengo wa matusi ya dhahiri!

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini