MAAMBUKIZI KATIKA VIUNGO VYA UZAZI VYA MWANAMKE-3

Wiki hii nitazungumzia matibabu na ushauri kuhusiana na tatizo hili. Matibabu mazuri hutegemea na uchunguzi makini wa awali, tatizo likiwa changa na kabla mwanamke hajaanza kutumia dawa mara kwa mara kwa tatizo hilo, hivyo basi, kwa umakini wa tiba unashauriwa uwaone madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama katika hospitali za mikoa ingawa uchunguzi na tiba za awali unaweza kupata katika vituo vya afya na hospitali za wilaya.

Lengo kuu la kuwahi tiba ni kuepuka kuharibu mfumo wako wa uzazi kwa kuziba mirija au mirija kujaa usaha au kujaa maji ambapo mwisho wake ni kupoteza uwezo wa kuzaa au ugumba.Aina ya tiba itakayotumika ni uamuzi wa daktari kama upate dawa mchanganyiko, ni za aina gani, daktari ataamua baada ya uchunguzi wa kina wa vipimo mbalimbali ambavyo tayari tumekwishaviona.

USHAURI

Unashauriwa kama unasumbuliwa mara kwa mara na ‘PID’ pia upime kama umeathirika na virusi vya HIV kwani na vyenyewe huchelewesha uponyaji. Tatizo hili au vimelea vya ugonjwa huu pia humuathiri mwanaume.
Mwanaume hulalamika maumivu katika njia ya mkojo na mkojo kuwa wa moto, kutokwa na majimaji katika njia ya mkojo na maumivu ya uume, kwa hiyo ni vema naye achunguzwe na kutibiwa.

PID inawatokea wasichana na wanawake watu wazima walio katika umri wa kuzaa, kwa hiyo unaweza kukuta msichana ambaye hana historia ya kupata ujauzito anapoolewa na kutafuta mtoto kwa mwaka mzima akakosa, akipimwa mirija akaambiwa imeziba, kumbe alishawahi kusumbuliwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu hapo siku za nyuma.

Mwanamke aliyekwishazaa naye anaweza kupatwa na tatizo hili. Tumeona kwamba mojawapo ya mambo yanayoeneza ugonjwa huu ni kupata damu ya hedhi kwa muda mrefu zaidi ya siku saba au kutokwa na damu ukeni bila ya mpangilio, kwa hiyo endapo una tatizo kama hilo basi waone madaktari wa akina mama kwa uchunguzi wa kina na tiba.

Jiweke katika hali ya usafi hasa ukeni na nguo za ndani, epuka magonjwa ya ngono na utoaji wa mimba. Zingatia kuhudhuria hospitali haraka unapohisi tatizo, usisubiri likawa kubwa, usitumie dawa bila ushauri wa daktari au bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina hospitali, mfano kupimwa kama tulivyoeleza hapo awali, pata lishe bora, epuka ngono zembe na ulevi au matumizi ya mihadarati.

Jenga tabia ya kupima afya ya uzazi mara kwa mara hasa kama upo katika umri mkubwa ili kuona kama umeshaanza kupata dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi, kama tulivyoelezea dalili zinafanana na katika hatua za awali saratani hii inatibika, uchunguzi wake unafanyika katika vitengo maalum kwenye hospitali za mikoa.

Endapo itathibitika mirija imeziba basi muone daktari wa magonjwa ya akina mama katika hospitali ya mkoa, utatibiwa na kurudia katika hali yako ya kawaida na kupata uwezo wa kuzaa.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …