CCM Watoa Tamko Kali Kuhusu Yanayodaiwa Kufanywa na UKAWA Tanga!
Chama cha Mapinduzi kinasikitishwa na kitendo cha wafuasi wa vyama vinavyounda UKAWA kupiga mawe na kutupa chupa, baadhi zikiwa na mikojo, kwenye Ofisi ya CCM Mkoa wa Tanga jana, tarehe 28 Septemba 2015, kabla na baada ya mkutano wao wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Tangamano, Tanga Mjini.
Kama ilivyo kawaida yetu miaka yote, CCM iliazimia kufanya kampeni za amani, zinazoheshimu sheria za nchi na utu wa wapinzani wetu. Hadi sasa, tumeweza kuwadhibiti wapenzi, washabiki na wanachama wa CCM wasifanye vitendo vya ufunjifu wa amani.
Tukio la Tanga sio la kwanza. Tarehe 27 Septemba 2015 viongozi wa UKAWA waliwapanga vijana, katika eneo la stendi ya Uyole, mkoani Mbeya ili wasimamishe msafara wa Mgombea wa Urais wa CCM na kumfanyia vurugu na kumpigia kelele ili wananchi wasimsikie vizuri. Ingawa Mgombea wetu alifanikiwa kukabiliana na hali hiyo, tunaamini kwamba huu sio ustaarabu.
Washabiki wa CCM pia wana uwezo wa kupanga na kufanya mambo haya, tena kwa ufanisi mkubwa zaidi. Lakini viongozi wa CCM wa ngazi zote wamekuwa wanawahimiza wasifanye mambo haya kwasababu CCM hatuamini kwamba hiyo ni njia sahihi ya kuomba ridhaa ya Watanzania kuliongoza taifa letu na pia, kwa kuwa sisi ndio tuliokabidhiwa na Watanzania nchi hii kuiongoza, tunafahamu dhamana yetu kubwa ya uongozi wa taifa na ulinzi wa amani ya taifa letu.
Tukio la Tanga la Ofisi ya CCM Mkoa wa Tanga kupigwa mawe limewaudhi na kuwakera wana-CCM na wapenda amani wote wa Tanga. Hata hivyo, tumewasihi wana-CCM wasilipize kisasi. Chama chetu kina dhamana ya uongozi wa nchi na ulinzi wa amani ya nchi yetu. Wenzetu dhamana hiyo hawana. Chama chetu kina uhakika wa kushinda na kushika dola, wenzetu wana uhakika wa kushindwa na wamekwishakata tamaa.
Tunawapongeza wana-CCM kote nchini kwa utulivu waliouonyesha katika kipindi chote cha kampeni. Tunawashukuru kwa kubaini na kutoyumbishwa na propaganda za wenzetu ikiwemo ya Tanga, kwamba mkutano wa Tanga uliahirishwa kwasababu watu walikuwa wengi.
Itakuwa ni mara ya kwanza katika historia kwamba mkutano wa kampeni unaahirishwa kwasababu ya wingi wa watu. Katika mikutano ya kampeni, ikiwemo ya CCM, na hata katika sherehe za kitaifa, baadhi ya watu huzidiwa nguvu na huhudumiwa na wahudumu wa huduma ya kwanza huku mikutano ikiendelea.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa wenzetu kutafuta kisingizio cha kutofanya mikutano ya kampeni. Mkutano wa kampeni ya UKAWA wa Geita pia waliuahirisha kwa kisingizio tofauti, kwamba jukwaa na vipaza sauti havikuandaliwa ingawa aliyetangaza kuahirisha alisimama jukwaani na akasikika na watu wote.
Mabadiliko wanayoyahubiri wenzetu yanaanza na kusema ukweli. Imefika mahali sasa wenzetu wa UKAWA wawaeleze ukweli Watanzania kuhusu mgombea wao kushindwa kuhutubia baadhi ya mikutano au kuhutubia kwa dakika 3 kuliko kuwahadaa kwa kutengeneza matukio na vioja ili kuficha mapungufu ya mgombea wao.
Tunarudia kuwataka viongozi wa UKAWA kuacha kupanga vurugu, kuharibu mali za CCM, na kutukana wana-CCM. Tunarudia kuwataka waache kauli zao za kuibiwa kura. Kauli hizo ni za kukata tamaa na kuwandaa watu kufanya fujo. Tunadi sera zetu na wagombea wetu kwa amani ili tuwape Watanzania fursa ya kuchagua kwa amani ili taifa liendelee kuwa la amani, umoja, utulivu na mshikamano mara baada ya uchaguzi.
Imetolewa na: January Makamba Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya TaifaMjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM 29.09.2015