Kipindupindu chazidi kuwa tishio, chapiga hodi Singida 11 walazwa
WAKATI ukiwa bado ukiendelea kutikisa katika Jiji la Dar-es-Salamu na kuua watu wengi, ugonjwa wa Kipindupindu umeingia katika Manispaa ya Singida ambapo watu 11 wamelazwa kwenye kambi iliyotengwa eneo la viwanja vya Mandewa kwa ajili ya kutibu wenye dalili za ugonjwa huo.
Tayari watu watatu miongoni mwa 11 waliozwa kwenye kambi iliyoanzishwa wakiharisha na kutapika, wamefanyiwa vipimo vya kitaalamu na kubainika kuwa na ugonjwa huo hatari wa kipindupindu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mganga mkuu wa halmashauri ya Manispaa ya Singida Dr John Mwombeki amesema kuwa ugonjwa huo umelipuka katika eneo lake baada ya kubainika kwa mgonjwa mmoja aliyerejea hivi karibuni kutoka Jijini Dar-es-Salaam.
Amesema baada ya kubainika kwa mgonjwa huyo mmoja na kuanzishwa kambi maalum ya kutibu kipindupindu watu wanaoharisha na kutapika wameendelea kuongezeka na kuleta tishio zaidi.
Hata hivyo amesema tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kukabiliana na ugonjwa huo huku akiwataka wananchi kuwa makini na kutoa taarifa wakati kunapo onekana dalili zozote za kuwapo kwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Ingawa wataalamu wanasema hatua zimechukiliwa lakini hali halisi mtaani inaonesha kuwa bado kuna haja ya elimu kwa wananchi ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo hatari wa kipindupindu.