Kutoka Mbeya, Tume ya uchaguzi yatoa kauli ya matumaini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imewahakikishia wananchi na vyama vya siasa kuwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu katika ngazi zote za Udiwani, Ubunge na Urais yatatolewa kwa wakati bila ya mizengwe yoyote.
NEC imesema imejipanga kuhakikisha kuwa hakuna ucheleweshaji wa matokeo yoyote ya uchaguzi huo kwa kisingizio cha changamoto za mfumo wa uingizaji matokeo kutoka vituoni.

Uthibitisho huo umetolewa jijini Mbeya na Afisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, anayeshughulikia masuala ya uchaguzi, Jane Tungu, wakati akizungumza na waandishi wa habari kando ya mafunzo ya siku mbili ya uendeshaji wa uchaguzi huo kwa Waratibu wa Uchaguzi wa mikoa ya Mbeya na Iringa, Wasimamizi Wasaidizi na Maafisa wa Uchaguzi wa halmashauri zote za mikoa hiyo.

Waratibu wa Uchaguzi huo kwa mikoa ya Mbeya na Iringa, wamewaondoa hofu wananchi kuwa kamwe hawatafanya upendeleo kwa chama chochote cha siasa kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa bali watazingatia kanuni, sheria na maadili ya uchaguzi yaliyowekwa na tume.
Awali akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amewataka Mawakala wa vyama vya siasa kutambua kuwa jukumu lao ni kuangalia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama zinatekelezwa ipasavyo, lakini hawapaswi kuingilia utendaji wa Maafisa wa tume na Wasimamizi wa uchaguzi huo.
Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu kote nchini kwa ngazi za Udiwani, Ubunge na Urais.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …