MAGUFULI Amlipua Mbunge wa CCM Huko Mbeya!

MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameahidi atakapochaguliwa kuwa rais, atarudisha sehemu ya mashamba ya Kapunga ya wilayani Mbarali katika mkoa wa Mbeya kwa wananchi.

Aidha, Magufuli ambaye amemlipua aliyekuwa Mbunge wa Mbarali kwa tiketi ya CCM, Modestus Kilufi, amesema akichaguliwa, pia mgogoro kuhusu Hifadhi ya Ruaha kati ya wananchi na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), utakoma na atakayebughudhi wananchi, atakiona.

Dk Magufuli alitoa ahadi hiyo jana katika mikutano aliyoifanya kwenye maeneo mbalimbali wilayani hapa. “Ninataka mashamba yarudi haraka kwa wananchi… Nikisema nimesema,” alisema aliposalimia wananchi katika eneo la Igurusi.
Alisema anafahamu vyema sheria za ardhi; mamlaka ya vijiji na ya matumizi ya ardhi. Alisema chini ya sheria ya mamlaka ya vijiji, Rais ana mamlaka ya kufanya mabadiliko hivyo atawarudishia wananchi ekari 1,800 zilizochukuliwa na mwekezaji.

Kwa mujibu wa Magufuli, mwekezaji aliomba ekari 3,000 na baadaye akaongezewa ekari 1,800 ambazo ndizo wananchi wamekuwa wakilalamikia kwa muda mrefu. Hata hivyo, Dk Magufuli alisema mchakato wa kurudisha ardhi hiyo ulishaanza, lakini ulikuta mwanaCCM aliyeaminika awali kwamba angetimiza maslahi ya wananchi, lakini ikawa tofauti.

Ingawa mgombea huyo hakutaja aliyekwamisha mpango huo, alimaanisha kwamba ni aliyekuwa Mbunge wa Mbarali, Kilufi ambaye baada ya kushindwa katika kura za maoni, alihamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya kukimbilia ACT Wazalendo ndani ya siku tatu.
“Ekari zingesharudi kwa wananchi, mmekwamishwa… kulikuwa na mtu tuliyemwamini… Watu wabaya hawako kwenye vyama vingine tu, hata CCM wamo,” aliuambia mkutano katika eneo la Chimala.
Akizungumzia maendeleo yaliyofikiwa, Magufuli alisema ni vyema Watanzania wakaelezwa ukweli kwamba siku zote changamoto haziwezi kumalizika mara moja. Alisisitiza kwamba, ni vyema Watanzania wakaelezwa ukweli juu ya hilo.
Alitoa mfano kwamba tangu awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere hadi awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, licha ya kufanya kazi nzuri, hawakumaliza chagamoto zote kama ambavyo pia yeye hawezi kumaliza zote.


Kuhusu hifadhi ya Ruaha, Magufuli alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alipokwenda kuutatua, alisema kuna vijiji 21 ambavyo viliingizwa kimakosa kwenye hifadhi. “Nataka niwahakikishie wana vijiji hivyo, anayefanya mabadiliko yoyote ni rais na wala si mbunge.

Na anayeongea hapa kwenu ndiye rais mtarajiwa,” alisema na kuhoji wananchi kama atakuwa rais wakamjibu ‘ndiye rais.’ Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela ametinga kwenye kampeni za kumnadi Dk Magufuli na kuponda Ukawa na wana CCM waliohama akiwaita waasi na walafi wa madaraka.
Malecela alipanda jukwaani jana katika mkutano wa kampeni wa Magufuli, mjini Rujewa, Mbarali mkoani Mbeya na kuhimiza wananchi waoneshe kwamba CCM aliyoiacha Mwalimu Julius Nyerere bado iko imara. “Kwa kifupi Ukawa ni kundi lenye makundi mawili.

La kwanza ni wapinzani ambao mwaka 1992 tuliwapa usajili, hata mara moja hawajatusumbua. Kundi la pili ni la waasi, wachoyo wa madaraka,” alisema Malecela. Aliendelea kuponda umoja huo wa Ukawa unaoundwa na Chadema, NCCR Mageuzi, NLD na CUF akisema ni kundi lisilo na sera. Alisema hicho si chama kwa sababu hawakuandikishwa kisheria.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini