MAGUFULI Selema Lelema Kila Kona!

02
Na Richard Bukos, Geita
AMSHA AMSHA! Wimbo maarufu wa ukakamavu wa ‘Selema Selema’ unaotumiwa na mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli (pichani) unatikisa kila kona ya Kanda ya Ziwa ambako waziri huyo wa ujenzi anazunguka kuomba kura kwa wananchi.

Kwenye mikutano yake ya kampeni katika maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Kagera, Simiyu na Geita, alitumia muda mwingi kumwaga sera kabla ya kupumzika jana Alhamisi kwa ajili ya Sikukuu ya Idd el Hajj na baadaye leo anatarajia kufanya mkutano mkubwa katika Uwanja wa Taifa wa Kahama mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya msafara huo, leo asubuhi, Dk. Magufuli atapita akimwaga sera katika vijiji vilivyo njiani kuelekea Shinyanga, kama ambavyo amekuwa akifanya maeneo mbalimbali ambako makundi madogomadogo ya watu yamekuwa yakimsimamisha njiani na kuwahutubia.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu mkoani Shinyanga, maandalizi kwa ajili ya mkutano huo yanaendelea vizuri na idadi kubwa ya watu wamekuwa wakijitokeza kuangalia namna mafundi mitambo wanavyoendelea na kazi ya kujenga majukwaa na kuseti mitambo.
Katika mikutano yake ndani ya kanda hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini, wananchi wamekuwa wakifurika na kuwapa kiwewe wapinzani. Kwenye mikutano hiyo, Dk. Magufuli amekuwa akiwaahidi wachimbaji wadogowadogo kuwa endapo atapata ridhaa ya kuwa rais, ataondoa utaratibu wa kuwafukuza kila eneo linapogundulika kuwa na madini kwa ajili ya kuwamilikisha wachimbaji wakubwa.

Mgombea huyo wa urais amesema endapo wachimbaji wadogo watagundua machimbo mapya, kazi ya serikali yake itakuwa ni kuwapa vibali vya kuyamiliki na kuwakopesha nyenzo za kufanyia kazi zao ili kuwanufaisha na endapo mtu atataka kuuza eneo lake kwa wafanyabiashara wakubwa, afanye hivyo kwa hiyari yake mwenyewe. Mkoani Kagera, Dk.Magufuli amewaahidi wakazi wa huko kuwajengea kiwanda cha mabati.

“Haiwezekani hapa kuwe na malighafi ya kutengenezea mabati halafu wananchi wasubiri yanayotoka Dar es Salaam. Mkinipa kura nitajenga kiwanda cha bati hapa ili mpate bidhaa hiyo kwa bei ya chini,” alisema.
Kabla ya kufika mkoani Shinyanga, Dk. Magufuli aliyeambatana na baadhi ya wajumbe wa kamati ya kampeni ya chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo ameshafanya mikutano ya kampeni maeneo kadhaa yakiwemo Chato, Biharamulo, Bukoba na Geita.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini